ARUSHA : Waasi wa Dafur wafikia msimamo wa pamoja
6 Agosti 2007Makundi ya waasi wa Dafur leo hii wamekamilisha mazungumzo yao katika mji wa Arusha nchini Tanzania kwa kukubaliana kuwa na msimamo wa pamoja ili kuweza kuingia kwenye mazungumzo ya mwisho ya amani na serikali ya Sudan hivi karibuni.
Msimamo huo wa pamoja kwa makundi hayo ya waasi unaonekana kuwa ni hatua nyengine muhimu katika kukomesha mapigano ya umwagaji damu ya zaidi ya miaka minne huko Dafur ikiwa ni wiki moja baada ya Umoja wa Mataifa kuamuwa kupeleka kikosi cha wanajeshi 26,000 kulinda amani huko Dafur.
Makundi manane ya waasi hao wa Dafur wamewasilisha msimamo wa pamoja juu ya kushirikiana madaraka na utajiri, mipango ya usalama, masuala ya ardhi na yale ya kibinaadamu kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho na serikali ya Sudan.
Pia wamependekeza kwamba mazungumzo hayo ya mwisho yanapaswa kufanyika kati ya miezi miwili hadi mitatu kuanzia sasa.
Hata hivyo mazungumzo hayo yamesusiwa na viongozi wawili wakuu wa waasi akiwemo baba muasisi wa uasi wa Dafur Abdel Wahid Mohammed Nur.