Arteta: Nina matumaini ya kubeba taji msimu huu
21 Agosti 2023Arteta anasema kwamba ana matumaini makubwa msimu huu kwa kuwa ana wachezaji wa kutosha tena walio bora. Ameyasema haya kuelekea mechi yao ya pili ya Ligi Kuu ya England watakayoicheza usiku wa Jumatatu ugenini, watakapowatembelea Crystal Palace katika uwanja wa Selhurst Park.
Kocha huyo vile vile amelalamikia ratiba iliyojaa mechi ya msimu huu akisema anawahofia wachezaji wake, kwani tayari kumeshuhudiwa majeraha mabaya ya goti miongoni mwa wachezaji katika timu tofauti.
Mmoja wa wachezaji walionunuliwa na Arsenal katika dirisha hili la uhamisho Jurrien Timber alijeruhiwa katika mechi ya kwanza wiki mbili zilizopita na atakuwa nje kwa miezi kadhaa.
Kevin De Bruyne wa Manchester City, Tyrone Mings na Emu Buendia wa Aston Villa na Thibaut Courtois na Eder Militao wa Real Madrid ni baadhi tu ya wachezaji waliopata majeraha makubwa yatakayowaweka nje kwa muda mrefu.
Chanzo: DPAE/APE/Reuters