1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Armenia yakataa upatanishi wa Urusi

Sekione Kitojo
30 Septemba 2020

Armenia imekataa upatanishi wa Urusi katika mzozo wake na Azerbaijan juu ya jimbo la Nagorny Karabakh, huku mapigano makali yakiendelea kwa siku ya nne.

https://p.dw.com/p/3jCa1
Berg-Karabach Konflikt
Picha: Defence Ministry of Armenia/Reuters

Armenia Jumatano imekataa pendekezo la Urusi la kutaka kuwa mpatanishi katika mazungumzo ya amani na hasimu wake mkubwa Azerbaijan, huku mapigano yakiwa yanaendelea kupamba moto kwa siku ya nne katika jimbo linalotaka kujitenga la Nagorno Karabakh.

Waziri mkuu  wa  Armenia Nikol Pashinyan amesema haitakuwa sahihi kufanya mazungumzo ya  amani  na Azerbaijan chini ya upatanishi wa  Urusi, wakati mapigano ya kuwania udhibiti wa jimbo yakiwa yanaendelea.

"Sio sahihi kabisa kuzungumzia kuhusu mkutano kati ya  Armenia, Azerbaijan na Urusi  katika wakati wa uhasama mkubwa," amesema Pashinyan wakati akizungumza na shirika la habari la Urusi Interfax.

Ameongeza kuwa hali endelevu na mazingira yanahitajika kwa ajili ya mazungumzo hayo. 

Vyombo vya habari nchini Urusi vimeripoti Jumatano kuwa waziri mkuu Pashinya amesema Armenia  haifikirii kuweka walinzi wa amani katika jimbo la Nagorno-Karabakh.

Kwa miaka kadgaa, vikosi vya Armenia na Azabajani vimekuwa vikizozania jimbo hilo la Karabakh, ambalo liliamua kutaka kujitenga na Azabajani baada ya kuanguka kwa Umoja wa Kisovieeti katika miaka ya 1990.

Mzozo huo wa muda mrefu uliibuka tena Jumapili huku pande hizo mbili zikirushiana silaha nzito za moto na kulaumiana kwa kuzuka kwa vurugu.

Karibu watu 100 wamethibitishwa kufa katika mapigano hayo ya hivi karibuni na pande zote mbili zinadai kuwa zimesababisha hasara kubwa kwa vikosi vya wapinzani.

Chanzo: afp