1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Argentina yaitambia Brazil katika Olimpiki

20 Agosti 2008

Vyombo vya habari vya Uingereza vimeendelea kutoa sifa kwa wanamichezo wake katika michezo ya Olimpiki mwaka huu, baada ya Christine Ohuruogu kutamba katika mbio za mita 400 wanawake.

https://p.dw.com/p/F1Ik
Sebastian Giovinco (10), wa Italy, na Alexandre Song, wa Cameroon,wanapambana kuwania mpira katika mashindano ya soka ya Olympic mjini Beijing hivi karibuni. Timu hizo zote zimetolewa katika robo fainali. Cameroon ilitolewa na Brazil na Itali ikatolewa na Ubelgiji.Picha: AP

Vyombo vya habari vya Uingereza leo vimemsifu Christine Ohuruogu kwa ushindi wake wa kushangaza katika mbio za mita 400 mjini Beijing, na kudokeza kuwa ushindi wake huo umekuwa mtamu zaidi kwa kuwa alibidi kupambana na mambo mengi kabla ya hapo.

Bingwa huyo wa olimpiki mwenye umri wa miaka 24 alitumikia adhabu ya mwaka mmoja ya marufuku mwaka jana kwa kukosa kufanyiwa uchunguzi wa madawa ya kuongeza nguvu mara tatu, lakini alipinga adhabu hiyo na kushinda kesi yake katika mahakama ya upatanishi ya michezo dhidi ya sheria ndogo ambayo inawapiga marufuku wanariadha ambao wamepigwa marufuku kwa ajili ya makosa ya kutumia madawa ya kuongeza nguvu.

Ohurougu alishinda kwa kutumia muda wa sekunde 49.69, akimshinda Shericka Williams wa Jamaica aliyetumia sekunde 49.69 wakati Sanya Richards aliyekuwa akipigiwa upatu kunyakua taji hilo kutoka Marekani akiwa wa tatu kwa kutumia sekunde 49.93. Ushindi wa Olimpiki wa Ohuruogu unaongeza jumla ya mataji aliyokwisha nyakua ikiwa ni pamoja na la dunia na commonwealth, ikiwa ni wiki tatu baada ya kutumikia adhabu ya kupigwa marufuku.

New Zealand imeshangilia ushujaa wa mwanariadha wake Nick Willis , ambaye ushindi wake wa medali ya shaba katika mita 1,500 ulikuwa ni ushindi wa kwanza wa nchi hiyo kupata medali ya olimpiki katika mashindano ya riadha katika muda wa miaka 32, wakati ikiangalia miaka ya enzi za kujivunia ya 1960 na 70 wakati New Zealand ilikuwa ikitamalaki mbio za masafa mafupi na ya kati.

Ni uzuri usio kifani, amesema bingwa wa zamani wa olimpiki kutoka New Zealand Peter Snell ambaye alishinda medali ya dhahabu katika mbio za mita 800 wanaume katika mwaka 1960 na 1,500 mwaka 1964, aliiambia radio New Zelanad, kuwa si tu kwamba ni shaba lakini shaba katika enzi za sasa.

Snell amesema kuwa ilikuwa vigumu kwa Nick , kwasababu hapo zamani kulikuwa hakuna Waafrika kama Walgeria, Wamorocco na Wakenya , ambao ni wanariadha ambao ni vigumu kuwashinda, na ameweza kufanya hivyo.

Medali ya shaba aliyonyakua Willis ni ya kwanza katika riadha kunyakuliwa na New Zealand tangu pale John Walker aliponyakua medali ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 mwaka 1976 mjini Montreal, kufuatia nyayo za Snell ambaye alimfuata Jack Lovelock aliyepata ushindi katika mbio hizo mwaka 1936 mjini Berlin.

Siku ya saba katika michezo ya olimpiki ya riadha mjini Beijing kesho Alhamis kutakuwa na michezo sita, lakini bingwa wa mbio za mita 110 Liu xiang wa China hatakuwapo kutokana na kuumia mguu na kujitoa katika mashindano hayo.

Mbali na mbio hizo za mita 110 kuruka viunzi, fainali ya mbio za mita 400 wanaume na mita 200 wanawake ni matukio makubwa katika burudani hii ambayo pia kutakuwa na mchezo wa kuruka triple jump fainali kwa wanaume na kurusha mkuki kwa wanawake ikiwa ni fainali.

Mchezo wa kutembea kilometa 20 ikiwa ni fainali umepangwa kufanyika kesho asubuhi. Pia kutakuwa na nusu fainali ya mbio za mita 800 wanaume na wanawake mita 1,500 kabla ya fainali zake zote kufanyika hapo Jumamosi, pamoja na mbio za mita 100 mara nne kupokezana vijiti , kwa wanawake ambapo fainali zake zitafanyika hapo Ijumaa.

Bingwa wa mbio za mita 100 Mjamaica Usain Bolt atakuwa ulingoni tena kwa ajili ya kuwania medali nyingine ya mbio katika muda wa miaka 24 leo Jumatano wakati zitakapofanyika fainali za mbio za mita 200 katika uwanja wa kiota cha ndege mjini Beijing.

Bolt , ambaye ametawala fainali za mbio za mita 100 kwa kuvunja rekodi ya dunia, amesema kuwa anadhani ushindi wa mbio zote hizo mbili kwa pamoja ambao mara ya mwisho mtu kushinda alikuwa shujaa wa Marekani Carl Lewis mwaka 1984 unawezekana , na kwamba anaweza kuonyesha maajabu tena.

Bingwa huyo mwenye umri wa miaka 21, Bolt anamiliki muda wa kasi mara tatu wa mita 200 msimu huu.

Pia katika mbio hizo Bolt atakuwa na upinzani mkali kutoka kwa Mmarekani Walter Dix, ambaye amenyakua medali ya shaba katika mbio za mita 100, Churandy Martina kutoka katika visiwa vya Uholanzi vya Antilles, Brian Dzingai kutoka Zimbabwe na Wallece Spearmon, ambaye alishinda medali ya shaba katika mbio za mita 200 katika mashindano ya dunia ya riadha mwaka jana.

Kwa jumla medali 11 zitashindaniwa katika michezo yote hii leo.

Wakati huo huo katika soka samba la Brazil lilidoda jana Jumanne na kutoa nafasi kwa mirindimo ya tango kushamiri dhidi ya timu ya soka ya Brazil wakati walipopoteza mchezo wao wa nusu fainali kwa mabao 3-0 dhidi ya mahasimu wao wakubwa Argentina.

Ni kulipiza kisasi kwa Argentina baada ya kupoteza fainali mbili za kombe la mataifa ya America ya kusini 2004 na 2007 pamoja na kombe la Confederation mwaka 2005 dhidi ya Brazil.

Kwa ushindi huo, Argentina pia imehakikisha kuwa timu ya Brazil haipati medali yake ya kwanza ya dhahabu ya olimpiki katika soka ambalo wanatawala kwa uhakika, baada ya kushinda mara tano ubingwa wa dunia. Inauma kufahamu kuwa hatuwezi tena kutafuta medali ya dhahabu ambayo tumekuja hapa kuitafuta, Alexandre Pato ameliambia shirika la habari la Ujerumani – Presse Agentur DPA.

Mshambuliaji kijana wa AC Milan akaongeza, nafahamu historia ya ushindani kati ya Brazil na Argentina, lakini nafikiri katika hali hii ilikuwa mchezo kati ya timu mbili kubwa ambamo timu iliyocheza vizuri imeshinda. Argentina ilistahili ushindi.

Pato alikuwa pekee miongoni mwa nyota wa Brazli ambaye aliweza kukabili kundi kubwa la waandishi wa habari ambao walihitaji maelezo kwa kile walichokiita kipigo cha kudhalilisha na maafa. Nyota Ronaldinho, ambaye aliitwa katika kikosi hicho cha olimpiki dakika za mwisho kwa msisitizo wa rais wa shirikisho la soka la Brazil , aliwakwepa waandishi wa habari na kuelekea katika sehemu ambayo alitakiwa kwa ajili ya uchunguzi wa madawa ya kuongeza nguvu.

Ripota mmoja hakupendezewa na mtazamo wa Ronaldinho. Alisema mwandishi huyo nataka kumuuliza Ronaldinho kwanini alimkumbatia sana Messi baada ya mchezo huo.

Hata hivyo Ronaldinho ambaye hakuwa katika hali nzuri kiuchezaji hakuna lengo kuu la hasira za waandishi habari wa Brazil.

Katika fainali ya soka la olimpiki, Argentina itapambana na Nigeria baada ya Nigeria nayo kuilaza Ubelgiji mabao 4-1.