Argentina na Uswisi na Ubelgiji na Marekani
1 Julai 2014Wakati huo huo mjini Salvador Marekani inaisubiri Ubelgiji katika pambano linalosubiriwa kwa hamu usiku.
Lionel Messi amekuwa ndio ufunguo wa mafanikio ya kikosi cha Argentina katika kombe la dunia, akipachika wavuni mabao manne kati ya sita ambayo Argentina imeyapata hadi sasa katika kinyang'anyiro hiki.
Pia wengine wanaowania kuingia katika robo fainali leo(01.07.2014) ni Marekani na Ubelgiji, timu ambayo imewasili katika mashindano haya ikitajwa kuwa moja ya timu zinazoweza kutoroka na taji hilo, lakini bado haijaonesha makali yake kamili.
Argentina haijafikia kiwango chake
Licha ya kuwa Argentina haijafikia kiwango chake kinachotarajiwa , Messi amekuwa katika sayari nyingine kabisa katika uchezaji wake, akiwavutia mashabiki na kuondoa kumbukumbu za ukame wa magoli uliomkumba kule Afrika kusini katika kombe la dunia mwaka 2010.
Mshambuliaji mwenzake Sergio Aguero hana hakika ya kuteuliwa kuingia dimbani hii leo baada ya kupata maumivu dhidi ya Nigeria katika mchezo wao wa makundi, hata hivyo , iwapo hatacheza kocha Alejandro Sabella huenda akaamua kumchezesha Ezequiel Lavezzi badala yake.
Uswisi inayopambana na Argentina ina matumaini kuwa Xherdan Shaqiri , ambaye amepewa jina la utani la Messi wa milima ya Alps kutokana na ufundi wake wa kutandaza kandanda, atakuwa muhimu kuweza kuishinda Argentina kwa mara ya kwanza.
Mchezaji huyo mwenye mwili mkakamavu yuko katika hali nzuri kimchezo , hasa alipowaduwaza Honduras kwa mabao yake matatu ambayo yamesaidia kwa Uswisi kuingia katika duru hii ya timu 16.
Ubelgiji inapigiwa upatu kutoroka na taji
Ubelgiji ilipata ushindi katika awamu ya makundi dhidi ya Algeria, Urusi na Korea kusini lakini hawakuwa katika hali yao ya juu, wakishindwa kufunga katika michezo mingi hadi katika dakika 20 za mwisho.
Lakini Kocha Marc Wilmots anatarajia mchezaji anayeichezesha timu Eden Hazard , mchezaji mwingine ambaye bado hajang'ara kuweza kufanya kile kinachokusudiwa, ili kuingiza ushawishi wake katika mchezo wa leo.
Baada ya kuzikaba koo Ureno na Ghana na kunyakua nafasi ya pili nyuma ya Ujerumani katika kundi la G , Marekani imeanza kupata kujiamini na inapanga kuendelea na mapambano.
"Hatuna hofu kabisa," kocha wa Marekani Juergen Klinsmann amesema. "Tuko katika hali nzuri, tumerejea katika hali yetu ya kawaida baada ya kila mchezo hadi sasa. Tunahisi kama tumeanza mchakato huu. Amesema Klinsmann.
Cameroon na madai ya kupanga matokeo
Wakati huo huo shirikisho la soka la Cameroon limeanzisha uchunguzi kuhusu madai ya kupanga matokeo dhidi ya baadhi ya wachezaji wake katika kombe la dunia. Madai hayo yanatokana na taarifa ya gazeti la Ujerumani la Der Spiegel.
Vyombo vya habari vya Cameroon vimeripoti kuwa nahodha wa Simba hao wa nyika Samuel Eto'o amehojiwa na majeshi ya usalama nchini humo kwa kuhusika na madai hayo.
Wakati huo huo kocha wa Nigeria Stephen Keshi amejiuzulu wadhifa huo baada ya nchi yake kuondolewa katika kinyang'anyiro cha kombe la dunia, FIFA imesema leo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre / afpe
Mhariri: Yusuf , Saumu