1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Argentina na ndoto yake

Maja Dreyer30 Oktoba 2007

Ziara ya Angela Merkel nchini India, uchaguzi wa rais mpya nchini Argentina na mjadala kuhusu kuweka kithibiti mwendo kwa barabara kuu hapa Ujerumani – hayo ndiyo masuala kutoka kwenye kurasa za wahariri.

https://p.dw.com/p/C7l7

Kwanzi juu ya ushindi wa Christina Kirchner kwenye uchaguzi wa rais huko Argentina ambaye atachukua wadhifa wa mume wake Nestor Kircher. Mhariri wa gazeti la “Fränkischer Tag” juu ya matumaini ya Waargentina:

“Ukoo wa Kirchner unaangaliwa kama uokozi wa taifa zima. Baada ya uchumi wa Argentina kufilisika mwanzoni wa karni hii, nchi hiyo imenusurika kutokana na kukua kwa uchumi chini ya rais Nestor Kirchner. Ndiyo maana, Waargentina wana matumaini makubwa kwamba Bi Cristina Kirchner atawaletea hata maisha bora zaidi. Lakini wasisahau kwamba Argentina kweli ilikuwa chini kabisa wakati Nestor Kirchner alipoingia madarakani, kwa hivyo iliweza tu kuimarika tena kiuchumi. Vilevile, matatizo mengi kama rushwa, kutokuwa na usalama na umaskini bado hayajatatuliwa.”

Katika gazeti la “Braunschweiger Zeitung” tunasoma kwamba ushindi huu si tu ushindi wa ukoo wa Kirchner. Limeandika:

“Bibi huyu mwanasheria anataka kubadilisha sera na kuboresha hali ya maskini wa Argentina. Pia kuna habari juu ya udanganyifu katika uchaguzi lakini hakuna anayetaka kuzisikia. Argentina inataka tu kufuata ndoto yake.”

India inazidi kupata umuhimu katika siasa za kimataifa, siyo tu kiuchumi bali pia kisiasa. Ujerumani labda imechelewa kuyatambua haya, anaandika mhariri wa “Tagesspiegel” la mjini Berlin, wakati Angela Merkel amewasili India kwa ziara yake. Mhariri basi anachambua India ina umuhimu gani:

“Nchi ambaoe inafanikiwa kuziunganisha tamaduni na dini mbalimbali ni muhimu sana kuhusiana na mizozo ya kimataifa. Tena inapaswa kuwa na mahusiano mazuri na nchi ambayo inachukua nafasi ya pili kwenye orodha ya nchi yenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu, pamoja na kuwa jirani wa Pakistan. Aidha, India ina umuhimu katika suala lingine ambalo Kansela Merkel analishughulikia, yaani utunzaji wa hali ya hewa. Ikiwa kutakuwepo makubaliano ya kimataifa, nchi kubwa kama India zinalazimika kubeba jukumu fulani. Basi, kama unataka kusaidiwa na nchi hiyo inabidi ichukuliwe kama mshirika.”

Na la mwisho tusikie maoni ya wahariri juu ya pendekezo la chama cha SPD cha hapa Ujerumani kuweka kithibiti mwendo kwa barabara kuu hapa nchini ambapo bado waendeshaji wanaruhusiwa kuenda mbio kama wanavyotaka. Mhariri wa “Abendzeitung” lakini anakiunga mkono chama cha SPD:

“Kuweka kithibiti mwendo cha kilomita 130 kwa saa ni wazo zuri. Kwanza kithibiti hiki kitasaidia kuzuia ajali, na pili kupunguza mbio kutapunguza pia utoaji wa gesi za magari.”

Gazeti la “Frankfurter Rundschau” linaangalia zaidi upande wa hisia za Wajerumani na linachambua kwamba kutokuwa na kithibiti mwendo ni muhimu sana kwa Wajerumani. Tunasoma:

“Kila kabila lina tabia moja mbaya katika maisha ya kila siku, jambo ambalo linazusha hisia kubwa. Wahispania wanapenda kuwaua mafahali hadharani. Waitalia wanapenda kula ndege wanaoimba na Wakorea wanakula mbwa. Sisi Wajerumani basi tunataka kwenda kwa kasi kubwa iwezekanavyo kwenye barabara kuu bila ya kujali gharama yake.”