Argentina huenda isifike Urusi mwakani
13 Oktoba 2017Brazil itafanyia mabadiliko kikosi chake kwa ajili ya michezo ya kuwania kukata tikiti kwa kundi la mataifa ya Amerika ya kusini , ambayo yaelekea Chile huenda ikakaa nje ya fainali hizo mwaka ujao. Kocha wa Brazil Tite alimtumia mlinda mlango Ederson na mlinzi Maeguinhos katika kikosi chake kikuu wakati wa mazowezi mjini Sao Paulo jana Jumapili.
Brazil inayoongoza michuano hiyo ya America ya kusini ilishakata tikiti yake tangu mapema mwezi Machi mwaka huu. Uruguay, Chile, Colombia, Peru, Argentina na paraguay bado zinategemea matokeo ya kesho Jumanne ili kujihakikishia uhai ama kufuzu katika fainali hizo.
Mshambuliaji wa Brazil Gabriel Jesus amesema timu yake haitaionea huruma Chile. "Tulicheza michezo mitatu ya kufuzu tangu tulipokata tikiti yetu kwenda Urusi na tabia ya kikosi chetu imekuwa ile ile ," amesema Jesus baada ya mazowezi. "tutacheza ili kushinda." ameongeza.
"Iwapo Chile iko katika hali hiyo, sio kosa letu, ni lao," Miranda alisema.
Argentina nayo imo katika hali mbaya , na inawezekana mashabiki wasimuone Lionel Messi katika fainali hizo. Argentina inakabiliwa na kibarua kigumu wakati itakapocheza na Ecuador katika mchezo mgumu utakaochezwa katika mita 2,850 kutoka usawa wa bahari ikiwa ni hali ngumu kwa wachezaji kucheza katika eneo ambalo hewa ni nyepesi mno na kukosa hewa ya kutosha.
Syria huenda ikafikia fainali za kombe la dunia
Syria iko ukingoni mwa kukata tikiti yake katika fainali za mwakani za kombe la dunia iwapo itaishinda Australia , baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza wa mchujo nchini Malaysia wiki iliyopita. lakini katika mchezo huo inabidi kuhimili mashabiki wa nyumbani wa Australia ili kuweza kuendelea kuwasisimua mashabiki wake. Kocha wa Australia Ange Postecoglou hata hivyo anapanga mbinu za kuwakatisha tamaa mashabiki wa Syria.
"Kile tunachofahamu ni kwamba iwapo tutashinda kesho , tutaingia katika duru ijayo na lengo letu ni kucheza kandanda letu, tunataka kucheza kwa nguvu, tunataka kushambulia, tunataka kuupeleka mpira kwa maadui zetu na kuwapa changamoto na hicho ndio tutakachokifanya."
Katika bara la Afrika jana ilikuwa shangwe na vigelegele kwa mashabiki wa Misri baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Congo, ambao umewapa tikiti ya kucheza katika fainali za kombe la dunia nchini Urusi kwa mara ya kwanza tangu miaka 28 iliyopita nchini Italia.
Kwa upande mwingine katika kundi hilo la E, limeingia katika mtafaruku baada ya Ghana iliyotoka sare ya bila kufungana na Uganda kudai kwamba refa wa mchezo huo aliwanyima bao pamoja na mkwaju wa penalti. Ghana sasa imeliomba shirikisho la kandanda duniani FIFA kufuta matokeo hayo na kuamuru mchezo huo urudiwe.
Nigeria yaenda Urusi
Nigeria imekuwa nchi ya kwanza ya Afrika kukata tikiti yake katika fainali za kombe la dunia mwakani baada ya kuishinda Zambia kwa bao 1-0.
Na katika mbio za marathon zilizofanyika jana Jumapili mjini Chocago Galen Rupp alikuwa Mmarekani wa kwanza kushinda mbio hizo katika muda wa miaka 15 na Muethiopia Tirunesh Dibaba akashinda mbio hizo kwa upande wa wanawake. Bingwa wa medali ya shaba wa Olimpiki alishinda mbio hizo za kilometa tano kwa muda bora wa masaa mawili, dakika tisa na sekunde 20, akikimbia marathon yake ya nne.
Bingwa mtetezi wa mbio hizo Abel Kirui wa Kenya alimaliza akiwa wa pili kwa kutumia masaa mawili, dakika 9 na sekunde 48 na Mkenya mwingine Bernard Kipyego alishika nafasi ya tatu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / ape / afpe / dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga