1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa akamilisha ziara DRC

Angela Mdungu
2 Septemba 2019

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres amekamilisha ziara yake mashariki ya Congo, kwa kutembelea kituo cha afya wanakotibiwa wagonjwa wa Ebola magharibi mwa mji wa Beni. 

https://p.dw.com/p/3OseZ
Demokratische Republik Kongo |  Antonio Guterres
Picha: AFP/Getty Images/A. Huguet

Katika ziara yake kwenye kituo hicho kilicho katika mji mdogo wa Mangina kilomita thelathini magharibi mwa mji wa Beni, Antonio Guterres aliwasihi manusura wa Ebola kuwahamasisha watu walio karibu nao, kutokuwaficha majumbani wagonjwa, ili kusaidia kuitokomezwa haraka homa ya Ebola. 

Baada ya kupokelewa na matabibu pamoja na manusura wa homa ya Ebola katika kituo cha afya wanakotibiwa wagonjwa wa homa hiyo, Guterres amewahutubia manusura wa Ebola katika kituo cha afya cha Mangina, na kutoa wito wa kusambaza ujumbe kuwa wote wanaofika katika kituo hicho wanaweza kupona. Amewataka pia wananchi kutoficha dalili za homa ya Ebola, muje, na kutumia fursa ya kuushinda ugonjwa wa Ebola kwa kupata tiba katika kituo hicho.

Kwa upande wake Gavana wa mkoa wa Kivu ya kaskazini Charly Nzanzu Kasivita, amewasihi watu wanaopinga uwepo na makali ya Ebola kuondokana na dhana hiyo potofu, na kufika kupata matibabu katika eneo lililotengwa kwaajili ya matibabu ya Ebola 

Usalama mdogo watajwa kuwa kikwazo katika kuikabili Ebola

Nayo hali ya usalama mdogo katika eneo hilo ikiwa ni moja wapo ya vikwazo katika mpango wa kukabiliana na Ebola, katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres, ameahidi kwamba patafanyiwa mageuzi katika utendaji kazi wa tume ya Umoja huo nchini DRC MONUSCO ili raia wapate kunufaika na uwepo wa tume hiyo, na kwamba hilo litakuwa mojawapo ya maswala yatakayojadiliwa katika mkutano baina yake na rais Félix Tshisekedi mjini Kinshasa.
 
Tume ya Umoja wa mataifa kwaajili ya kustawisha amani katika DRC, ndio tume kubwa ya Umoja huo duniani na iliyo na vifaa tosha, lakini imekuwa ikilaumiwa na raia nchini humo kwamba haijafanya vyema katika utendaji kazi wake, hasa kuyatokomeza makundi ya waasi katika mji na wilaya ya Beni na kubwa kuliko yote likiwa ni lile la ADF kutoka Uganda, linalotajwa kuhusika na mauwaji ya watu zaidi ya elfu mbili katika eneo hilo kwa kuwakata kwa mapanga pamoja na risasi. 

Mwandishi: John Kanyunyu DW Mangina.