1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Annan aitaka serikali na upinzani Kenya utaje wajumbe leo

29 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CyzZ

Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, anaitaka serikali ya Kenya na upinzani nchini humo uwataje wajumbe watakaoshiriki katika mazungumzo ya kujaribu kukomesha machafuko ya kikabila ambayo tayari yamesababisha vifo vya watu takriban 800.

Wafuasi wa rais Kibaki wakiwa wamejihami na mapanga wamekuwa wakipigana na wafuasi wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga katika mkoa wa bonde la ufa tangu mwishoni mwa juma lililopita katika machafuko mapya yaliyosababishwa na matokeo ya uchaguzi wa tarehe 27 mwezi Disemba mwaka jana.

Watu wengine 32 waliuwawa jana huku shughuli zikikwama katika sehemu nyingi za Kenya.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ameutaka Umoja wa Afrika usimtambue rais Kibaki, lakini waziri wa mashauri ya kigeni wa Kenya, Moses Wetangula, anayehudhuria kikao cha umoja huo mjini Addis Ababa Ethiopia, amesema umoja huo hauna sababu ya kutomtambua Kibaki kama rais wa Kenya.

Raila Odinga na waziri wa Uingereza anayehusika na maswala ya Afrika, Mark Malloch- Brown, wametoa mwito kuwe na utulivu huku juhudi za kuutanzua mgogoro wa kisiasa nchini Kenya zikiendelea.

Marekani imewatolea mwito viongozi wa Kenya wafanye kila jitihada kufikia makubaliano. Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Marekani, Sean Mc Cormack, amesema amekuwa akiwasiliana na Kofi Annan ambaye bado yumo mjini Nairobi, lakini akadokeza kwamba mjumbe maalumu wa Marekani katika mzozo wa Kenya, Jendayi Frazer, hana mpango wa kurejea nchini humo katika siku za hivi karibuni.

Sambamba na hayo rais mstaafu wa Kenya, Daniel Torotoich arap Moi, alilazwa jana katika hospitali ya Nairobi kutokana na maumivu makali ya mgongo.

Daktari wake, David Silverstein, amesema hali yake ni nzuri na ataruhisiwa kuondoka hospitalini kesho Jumatano.