1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ANKARA:Marekani kushirikiana na Iraq,Uturuki na Iran kuhusu waasi wa PKK

2 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/C7AS

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi Condoleeza Rice anakutana na Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na maafisa wengine wa ngazi za juu ikiwa ni juhudi za kuzuia shambulizi la moja kwa moja kati ya Uturuki na eneo la kaskazini mwa Iraq.Mashambulizi hayo yanalenga kupambana na waasi wa kundi la PKK.Marekani inahofu kuwa uvamizi katika eneo la mpakani huenda ukayumbisha eneo la kaskazini mwa Iraq lililo na utulivu aidha kusababisha ghasia katika mataifa mengine yaliyo na waasi wa Kikurdi.

''Sote tunahitaji kuongeza nguvu juhudi zetu na Marekani ina hamu kubwa ya kufanya hilo kwani tunahitaji mpango wa pamoja ili kupata suluhu ya tatizo hili.Tumeshaanza kujadilia baadhi ya masuala nyeti ya mpango huo.Tatizo hili si la Uturuki ni la Iraq na Marekani vilevile.''

Uturuki kwa upande wake inashikilia kuwa inataka Marekani kuchukua hatua kali dhidi ya waasi wa PKK la sivyo kufanya mashambulizi. Hapo jana Uturuki ilianza kutekeleza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya kundi la waasi la PKK ili kuyumbisha shughuli zao.

Bi Condoleeza Rice na Waziri Mkuu Erdogan wanakutana kukiwa na ulinzi mkali huku maafisa alfu 2 wa polisi wakishika doria kwenye barabara za mji.

Waandamanaji wachache walikusanyika karibu na afisi kunakofanyika mkutano huo ila hakuna ghasia zozote zilizoripotiwa.Kundi kubwa la waandamanaji 200 lililoandaliwa na chma kidogo cha Kikomunisti cha Uturuki lilikusanyika mjini Istanbul huku wakitoa kauli za kuikashifu Marekani.