ANKARA: Uturuki imeahidiwa msaada kupambana na PKK
3 Novemba 2007Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani,Condoleezza Rice ameahidi kuisaidia Uturuki katika vita vyake dhidi ya chama cha Kikurd PKK kilichopigwa marufuku.Baada ya majadiliano yake pamoja na Waziri Mkuu Recep Tayyip Erdogan na Waziri wa Nje Ali Babacan wa Uturuki,Bibi Rice alisema,PKK ni adui wao wote.
Maelezo zaidi ya msaada huo yatajadiliwa siku ya Jumatatu pale Waziri Mkuu Erdogan atakapokutana na Rais George W.Bush wa Marekani mjini Washington.
Wanamgambo wa PKK huitumia kaskazini ya Irak kuishambulia Uturuki.Sasa Uturuki imepeleka kiasi ya wanajeshi 100,000 kwenye mpaka wake na Irak, ikijitayarisha kwa uwezekano wa kuvishambulia vituo vya wanamgambo wa PKK kaskazini mwa Irak. Washington na Baghdad zimetoa mwito kwa Ankara kutochukua hatua ya kijeshi kwa hofu kuwa itasababisha machafuko katika eneo pekee lenye utulivu wa aina fulani nchini Irak.