Angela Merkel akutana na Helmut Kohl
26 Septemba 2012Kansela Merkel atatowa hotuba katika makumbusho ya historia ya Ujerumani mjini Berlin, kwa heshima ya mkongwe wa siasa za Ujerumani Kohl mwenye umri wa miaka 82, kawa mchango wake wa kuleta muungano wa Ujerumani kwa amani na nafasi yake katika kujongeleana kwa bara la Ulaya. Wachambuzi wanasema siku ya leo pia itakuwa ni kumtukuza Kansela wa zamani kwa kumteuwa Merkel kuwa mrithi wake wa kisiasa na kwamba alikuwa mtu sahihi wa kuendeleza siasa zake.
Gazeti la Sueddeutsche Zeitung liliandika kwamba kwa kuzingatia shaka shaka na upinzani kuhusu mpango wa kuiokoa sarafu ya euro miongoni mwa wana Christian Democratic Union, ni muhimu kuwakumbusha watu kwamba euro ilizaliwa wakati wa enzi ya Kansela wa Ulaya Helmut Kohl.
Ingawa Merkel ni mwanasiasa maarufu kabisa nchini Ujerumani na anayetarajiwa na wengi kushinda uchaguzi mkuu mwaka ujao kwa mhula watatu, hata hivyo anakosolewa kwa kutokuwa na dira ya kuliongoza kundi la mataifa 17 wanachama wa sarafu ya euro kuweza kujitoa katika msukosuko mkubwa kabisa wa kiuchumi katika historia yake.
Kohl ni Kansela wa muungano
Kamishna wa zamani wa Ulaya Guenther Verheugen kutoka chama cha upinzani cha Social Democrats anasema Kohl alikuwa mwanasiasa wa aina ya pekee aliyekuwa mhimili wa Ulaya.
Merkel mwenye umri wa miaka 58 alilazimika kuvumilia kukosolewa na wabunge katika serikali yake mwenyewe ya mseto kati ya chama chake CDU/CSU na waliberali - chama cha FDP, kuhusiana na mpango wa kuiokoa euro. Kansela wa zamani Kohl ambaye sasa anatembelea kigari kutokana na uzee na akiwa amedhoofika kauli, amekuwa katika hali mbaya ya afya tangu alipopoza taya baada ya kuanguka.
Kohl aliacha kujihusisha na siasa 2002. Lakini ushawishi wake bado unaonekana katika safu za madaraka mjini Berlin, ambako anafahamika kama "Kansela wa Muungano," licha ya kashfa kadhaa zilizomkumba katika miaka ya baadae ya utawala wake.
Merkel na Kohl walikuwa na uhusiano wa karibu wa kikazi
Mnamo siku ya Jumanne Kohl alishiriki kwa mara ya kwanza katika mkutano wa kundi la wabunge wa CDU, ambapo Merkel pia alihudhuria, ikiwa ni kusherehekea Kohl alipochaguliwa kuwa Kansela tarehe 1 Oktoba ,1982.
Merkel likulia katika Ujerumani Mashariki ya Kikoministi na kujifunza siasa akiwa katika kivuli cha Kohl na akajiunga na Baraza lake la mawaziri ambapo akimwita "Binti yangu."
Ilikuwa mwaka 1999 baada ya miaka 16 ya utawala wake na jaribio la kutaka kumng'oa kwenye uongozi ndani ya chama cha CDU baada ya kukiongoza chama kwa nusu karne, ndipo Merkel alipofanikiwa kushika hatamu na kumrithi Kohl.
Sakata hilo lilitoakana na kashfa iliomuandama Kohl kuhusu upokeaji fedha zilizotolewa kwa chama chake na kukataa kuwataja waliochagia. Pamoja na hayo kwa mtazamo wa jinsi anavyoongoza Kansela Merkel anaiga mikakati ya Kohl mtu aliyemjenga kisiasa.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/afp
Mhariri: Mohammed Khelef