Merkel ajadili mabadiliko ya tabianchi, mahojiano na DW
8 Novemba 2021Ingawa Merkel amezungumzia mambo anayojivunia kuyafanikisha akiwa kansela, kama vile kuendeleza uhisano wa karibu na washirika wa Ujerumani, na kuanzisha mchakato wa Ujerumani kusita kutegemea makaa ya mawe, lakini pia hakuona aibu kutaja mambo ambayo angetamani kuwa ameyafanya vizuri zaidi.
Merkel amesema rekodi ya Ujerumani kuhusu suala la mazingira sio mbaya ikilinganishwa na nchi nyingine. Lakini pia amekumbusha kwamba Ujerumani ni mojawapo ya nchi zinazoongoza kiviwanda, kiteknolojia na kisayansi, hivyo ina wajibu wa kuongoza kwa mfano.
Soma zaidi:COP26 yaanza kuonyesha mafanikio
Kuhusiana na mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi unaofanyika mjini Glasgow wa COP26 Merkel amesema anawashawishi vijana wamendelee kuwashinikiza viongozi wao kuchukua hatua za haraka zaidi.
"Tunapaswa kuzingatia tena makadirio ya kisayansi, na hiyo inamaanisha kushikilia msimamo wetu wa ongezeko la joto la nyuzi joto 1.5 . Mkutano wa Glasgow tayari umeshafanikisha mambo kadhaa. Lakini hii bado ni kasi ya polepole sana kwa mtazamo unaoeleweka kwa vijana," amesema Merkel.
Yaliotokea Afghanistan "yanahuzunisha"
Kuhusu yaliotokea nchini Afghanistan kansela huyo amesema amehuzunishwa sana kwa Ujerumani kushindwa kufikia malengo waliyoyapanga ambayo ni pamoja na kupatikana kwa utaratibu wa kisiasa unaojitegemea, wasichana kuweza kwenda shule, wanawake kuwa na uhuru wa kutimiza ndoto zao na amani ya kudumu nchini humo.
Alipoulizwa ni changamoto gani mbili kubwa alizokabiliana nazo wakati wa uongozi wake wa miaka 16, Merkel amesema ya kwanza ni kuwakaribisha wakimbizi wapatao milioni moja waliokuwa wakikimbia vita Syria mnamo mwaka 2015. Na ya pili ni janga la hivi karibuni la ugonjwa wa COVID-19. Ameeleza kwamba migogoro hiyo miwili ilimgusa zaidi kwavile idadi kubwa ya maisha ya watu ilikuwa hatarini.
Hivi karibuni Merkel alihudhuria mkutano wake wa mwisho wa G20 wa nchi zilizostawi kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi akiwa pamoja na Olaf Scholz anaetarajiwa kumrithi ukansela. Je, alifanya hivyo ili kuwahakikishia washirika wake kuwa Scholz akichukuwa wadhifa wa ukansela Ujerumani itaendeleza uthabiti wake kwenye uwanja wa kimataifa?
Soma zaidi: Miaka mitano tangu maelfu ya wakimbizi walipoingia Ujerumani
Merkel amejibu hakupanga hivyo ila Scholz alihudhuria mkutano wa G20 kama waziri wa fedha wa Ujerumani. Lakini amesema alimkaribisha kushiriki nae mikutano ya faragha na washirika tofauti ili amtambulishe kama kansela mtegemewa ajae wa Ujerumani.
Na alipoelezwa kuwa itakua vigumu kumuona mtu mwengine kwenye kiti cha ukansela kufuatai uongozi wake wa miaka 16, Merkel alijibu huku akitabasamu kuwa baada ya muda watu watazoea.