1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Angela Merkel aelekea Uturuki

MjahidA25 Februari 2013

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, yuko nchini Uturuki kwa ziara ya siku mbili. Kando na kuzungumzia mgogoro wa Syria, katika ziara yake hiyo, Merkel pia atajadili swala la Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/17lBE
Merkel aondoka kuelekea Uturuki
Merkel aondoka kuelekea UturukiPicha: picture-alliance/dpa

Hii leo kansela huyo wa Ujerumani, Angela Merkel, anatarajiwa kukutana na waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, pamoja na rais Abdullah Gul na maswala ambayo yatajadiliwa katika mkutano huo ni mgogoro wa Syria na nia ya Uturuki kuomba uanachama katika Umoja wa Ulaya.

Kando na kuwa Ujerumani imekataa ombi la Uturuki kujiunga na nchi nyengine 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya, Merkel amesema sasa uwezekano huo unaweza kuwepo baada ya majadiliano ya kina.

"Naunga mkono haja ya kuufungua ukurasa mpya katika mazungumzo haya ili tuweze kusonga mbele. Nafikiri nitalizungumzia suala hili na serikali ya Uturuki wakati wa ziara yangu" Amesema Merkel.

Kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Getty Images

Juhudi za Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya zimepingwa katika siku za hivi karibuni kutokana na nchi hiyo kuwa na uhasama wa miaka mingi na Cyprus na pia upinzani mkali kutoka kwa wanachama wengine wa Umoja wa Ulaya.

Merkel atembelea vikosi vya ujerumani Uturuki

Jana jioni kansela Merkel alipowasili Uturuki, alifululiza moja kwa moja hadi katika eneo la Kahramanmaras kuvitembelea vikosi vya Ujerumani vilivyo huko tangu mwezi wa Januari mwaka huu.

Takriban wanajeshi 300 wa Ujerumani ni sehemu ya wanajeshi wa kikosi cha Jumuiya ya Kujihami ya NATO wanaoilinda Uturuki dhidi ya mashambulizi ya makombora kutoka Syria kufuatia ghasia zinazoendelea nchini humo.

Jeshi la Ujerumani
Jeshi la UjerumaniPicha: AP

Merkel amesema kamwe hawatawaruhusu watu kuvuka mpaka kutoka Syria kuingia Uturuki kueneza ghasia. Amesema ni muhimu kuwapa uhakika watu wanaoishi katika upande wa Uturuki kwamba watalindwa, na pia ni muhimu kutoa ishara iliyo wazi kwa wale waliopo katika upande mwingine wanaojaribu kuvuka mipaka na kuuleta mgogoro katika upande wa Uturuki, kwamba kitendo hicho hakitakubalika.

Kansela wa Ujerumani atakamilisha ziara yake nchini Utuiruki kwa kuhudhuria mkutano wa uchumi kati ya Ujerumani na Uturuki.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/dpa

Mhariri Josephat Charo