1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ancelotti: Madrid iko sawa kuonekana wanyonge dhidi ya City

26 Aprili 2022

Meneja wa Real Madrid Carlo Ancelotti amesema amefurahi kuwa klabu hiyo imefika nusu fainali ya ligi ya mabingwa licha ya ukosoaji na kikosi chake kukatishwa tamaa mwanzoni mwa msimu.

https://p.dw.com/p/4AS2n
Champions League 2021 Real Madrid vs Sheriff Tiraspol
Picha: Action Plus/picture alliance

Mabingwa hao mara 13 wa Champions League, wanajiandaa kucheza na Manchester City katika mechi ya mkondo wa kwanza siku ya Jumanne.

"Bado nakumbuka wakati wachambuzi walivyokuwa wakitukosoa mwanzoni mwa msimu,” Ancelloti aliuambia mkutano wa wanahabari katika uwanja wa Etihad mjini Manchester.

"Kuna timu mbili kwenye nusu fainali ambazo kila mtu alikuwa amezikatia tamaa-Real Madrid na Villareal.”

Villareal itamenyana na Liverpool ugani Anfield katika mechi ya mkondo wa kwanza itakayochezwa kesho Jumatano 27.04.2022.

Ancelotti amesema kuna hisia mseto miongoni mwa wachezaji wa Real Madrid- furaha lakini vile vile wasiwasi kutokana na mchezo dhidi ya mpinzani imara Manchester City.

"Historia yetu, baada ya kushinda mataji 13 ya Champions League, imewajengea mazingira mazuri wachezaji wetu na kuwapa motisha ya kufanya vizuri katika mechi za ligi ya mabingwa,” Ancelotti amesema.

Hata hivyo kuna mashaka juu ya kupatikana kwa wachezaji watatu katika mechi ya leo. David Alaba, Ferland Mendy na kiungo Casemiro huenda wakaikosa mechi hiyo kutokana na majeruhi.