1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ancelotti: Bale atacheza dhidi ya Villareal

13 Septemba 2013

Baada ya sakata la muda mrefu la uhamisho ambao ulimfanya kuwa mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi ulimwenguni, Gareth Bale hatimaye ataichezea Real Madrid mchuano wake wa kwanza dhidi ya Villarreal.

https://p.dw.com/p/19hHR
Gareth Bale alijiunga na Real Madrid akitokea Tottehman Hotspurs ya England
Gareth Bale alijiunga na Real Madrid akitokea Tottehman Hotspurs ya EnglandPicha: Reuters

Kumekuweko na shaka kuhusu kama Bale angecheza kwa sababu amecheza tu muda wa nusu saa kufikia sasa msimu huu, katika kichapo ilichopata timu yake ya Wales cha magoli matatu kwa sifuri mikononi mwa Serbia. Hata hivyo kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti amesisitiza kuwa atapata fursa kidogo ya kucheza katika mpambano huo mkubwa baina ya vigogo hao wawili kati ya wanne ambao bado wana rekodi ya asilimia 100 katika ligi kufikia sasa msimu huu. Ancelotti amesema ataamua kama Bale atacheza kuanzia kipindi cha kwanza ama cha pili.

Muitaliano huyo pia amemaliza uvumi kuhusu nafasi atakayocheza Bale katika kikosi cha Real kwa kusema kuwa anamwona akichezea upande wa kulia wa safu ya mashambulizi.

Barcelona, Madrid na Atletico zinatafuta matokeo ya ushindi kabla ya kuanza mechi za awamu ya makundi ya Champions League katikati ya wiki ijayo. Barcelona wanacheza na Sevilla, wakati Atletico Madrid wakichuana na Almeria. Waakti huo huo, wawakilishi wengine wa Uhispania katika Champions League Real Sociedad pia wanacheza leo ugenini dhidi ya Levante.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman