1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ofisi yake imeeleza kusikitishwa na uamuzi huo

13 Oktoba 2017

Ni baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi Rais Zuma kujibu mashtaka karibu 800 ya rushwa zikiwamo tuhuma za ununuzi tata wa silaha kutoka Ufaransa. Mashtaka mengine ni mahusiano yake na familia ya Gupta.

https://p.dw.com/p/2lnug
Südafrika Kapstadt Jacob Zuma Präsident
Picha: picture-alliance/dpa/N. Bothma

Saa chache baada ya Mahakama ya Rufaa Afrika Kusini kutoa uamuzi kuwa Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma hana budi kujibu mashtaka ya rushwa na ubadhirifu yanayomkabili, baadhi ya wanachama wa ANC wameshauri kiongozi huyo ajiuzulu ili kulinda heshima ya chama hicho.

 Zuma anaendelea kuongoza katika muhula wake wa pili utakaomalizika  2019.

 Hata hivyo, ofisi ya rais Zuma imeeleza kusikitishwa kwake na uamuzi huo na kusema kuwa  wataendelea kupambana ili rais huyo asishtakiwe huku wakisisitiza kuwa wanatarajia uamuzi wa haki utafanywa.

Kadhalika chama kikuu cha upinzani , Democratic Alliance kimesisitiza kuwa kitamuandikia Mwendesha Mashtaka mkuu wa Serikali ili kuhimiza Rais Zuma apelekwe mahakamani kujibu mashtaka hayo.

``Kama rais hana hatia kama anavyodai, basi aiache mahakama ithibitishi usafi wake,`` amesema Mmusi Maimane, Kiongozi wa DA.

Awali, Wakili wa serikali, aliyaweka pembeni madai hayo yaliyotolewa Aprili 2009  na kumpa Zuma nafasi ya kuendelea kuwania urais wa nchi hiyo. Zuma alikuwa akikabiliwa na madai  zaidi ya 780 ya rushwa.

Rais Zuma  na Mamlaka ya Mashtaka ya Taifa, (NPA) walikata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama kuu uliochukuliwa Aprili 2016.

Hata hivyo jaji Lorimer Leach alikataa uamuzi huo  na kusema si sahihi  kwa   NPA kuziweka pembeni tuhuma hizo.

Südafrika Mmusi Maimane
Picha: imago/Gallo Images

 Nafasi ya NPA katika kesi ya Zuma

NPA ina wajibu wa kuamua iwapo itaendelea na mashtaka hayo yanayohusiana  na ubadhirifu wa karibu dola 2 bilioni za  ununuzi tata wa silaha uliogharimu mlipa kodi mabilioni ya dola  kutoka shirika moja la Ufaransa.

Hata hivyo haikufahamika mara moja iwapo Zuma atakwenda katika Mahakama ya Katiba kujaribu tena kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu.

NPA inatakiwa kutilia maanani uamuzi wa msemaji wa Serikali, Luvuyo Mfaku aliyehimiza muda wote kuheshimiwa kwa sheria na kuzingatia maslahi ya utawala wa sheria.

Jaji Leach alisema: `` Ni vigumu kuelewa kwa nini utawala wa sasa wa NPA  umechukulia kuwa uamuzi wa kutengua mashtaka hayo unaweza kutetewa,``

 Kashfa hizo za rushwa dhidi ya Zuma tangu aingie madarakani zimejikita zaidi katika barua pepe zilizovuja zikihusisha pia familia ya Gupta, biashara za marafiki wa rais huyo  ambao wanadaiwa walitumia nafasi hiyo kupata mikataba minono katika kampuni zao.

Mwandishi: Florence Majani(Rte/Ap)

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman.