1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Anayedhaniwa kuwa mkuu wa Al-Qaeda Afrika Mashariki, auawa

11 Juni 2011

Anayedhaniwa kuwa mkuu wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda Afrika Mashariki, Fazul Abdullah Muhammad, ameuawa mjini Mogadishu.

https://p.dw.com/p/11YjK
Ubalozi wa Marekani baada ya kushambuliwa mwaka 1998Picha: AP

Polisi wa Kenya ameyasema hayo leo akithibitisha ripoti zilizotolewa na kundi la waasi la Somalia la al-Shabaab. Kamishna wa Polisi nchini Kenya, Mathew Iteere ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wamepokea taarifa hizo kutoka kwa viongozi wa Somalia.

Iteere amesema wameambiwa kuwa kuna magaidi wawili wameuawa Jumatano iliyopita nchini Somalia. Kamishna huyo wa polisi wa Kenya amesema mmoja wa watu hao ametambulika kama Fazul Muhammad.

Mapema, kamanda wa ngazi ya juu wa al-Shabaab alisema kuwa mmoja kati ya watu hao ambaye ameauawa karibu na Mogadishu ni Fazul Abdullah.

Fazul, aliyekuwa na umri wa miaka 38 anadhaniwa kupanga mashambulio ya kigaidi kwenye balozi za Marekani Dar es Salaam, Tanzania na Nairobi, Kenya mwaka 1998 ambapo zaidi ya watu 200 waliuawa na wengine walijeruhiwa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)
Mhariri: Mohamed Dahman