Amnesty yataka Afghanistan kuwaachia wanaharakati 2
3 Februari 2024Shirika la utetezi wa haki za binaadamu la Amnesty International limetoa wito wa kuachiwa mara moja bila ya masharti wanaharakati wawili wa elimu wa Afghanistan ambao walikamatwa na vikosi vya usalama vya Taliban katikati mwa Oktoba mjini Kabul.
Soma taarifa hii: Afghanistan yahimiza mazungumzo na jamii ya kimataifa
Katika taarifa yake iliyotolewa Ijumaa jioni, Amnesty International imedai, Ahmad Fahim Azimi na Seddiqullah Afghan, wanaharakati wanaofanya kazi na shirika la elimu Fekre Behtar, wamekamatwa kiholela.
Tangu kurejea madarakani, serikali ya Taliban inatajwa kubinya haki za watu nchini humo. Shirika, Amnesty liliongeza kwa kusema kukamatwa kwa watu hao ni kinyume na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu.
Nchini Afghanistan wasichana na wanawake hawaruhusiwi kusoma zaidi ya shule ya msingi na vikosi vya Taliban vinalaumiwa kwa ukandamizaji dhidi ya wapinzani.