1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty International yatoa wito kuachiwa kwa mateka waliotekwa na Kundi la LRA huko Afrika ya Kati.

Scholastica Mazula22 Aprili 2008

Shirika la Kimataifa la kutetea haki za Binadamu-Amnesty Internation, limesema kwamba nchi za Afrika ya Kati zinatakiwa kuhakikisha kuwa mamia ya watu waliotekwa nyara na Waasi wa Uganda wanaokolewa.

https://p.dw.com/p/DmJG
Mwanajeshi mtoto wa kundi la Lord's Resistence Army-LRA, Samuel Okumu, akiwa ameshika bunduki amesimama kwenye mpaka wa Sudan na Kongo-DRC July 28, 2006.Picha: AP

Kwa mujibu wa Amnesty International, kiasi cha watu mia tatu na hamsini wakiwemo wanaume, wanawake na watoto wametekwa nyara hivi karibuni na kundi la waasi wa Uganda la Lord's Resistance Army-LRA.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema utekwaji nyara huo ulifanyika katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati,nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo -DRC na Kusini mwa Sudan sehemu ambayo waasi walikuwa wakijiandaa kwa ajili ya kutiwa saini makubaliano na Serikali ya Uganda kwa lengo la kumaliza vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka ishirini.

Mtafiti wa masuala ya Afrika ya Kati wa shirika la Amnesty Godfrey Byaruhanga anasema hilo ni jukumu lako kuhakikisha watu hao wanaokolewa.

Anasema Hatua waliyoichukua ni kukusanya taarifa zote kuhusiana na utekwaji huo uliofanywa na kundi la Lord's Resistance Army katika nchi tatu za Afrika ya Kati.

Wanajitahidi pia kufahamu ni wapi watu hao wamefichwa japo kuwa ni kazi ngumu ndiyo maana toa wito kwa Serikali za nchi husika kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanawaokoa watu hao wakati huohuo wakitoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuzisaidia nchi hizo ziwaokowe watu wake waliotekwa na kundi la LRA.

Taarifa ya Amnesty International inasema kwamba nchini Uganda mateka hao wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto huenda wakatumiwa kama wapiganaji watoto na watumwa wa ngono.

Mpaka sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na Serikali yeyeto za kujaribu kuwaokoa watu hao.

Lakini Serikali na Viongozi wa Afrika wanatakiwa kufanya nini ili kukomesha mpigano hayo ya muda mrefu katika eneo hilo Mtafiti wa Amnesty Godfrey Byaruhanga anasema wanadhani mgogoro huo wa muda mrefu utamalizika tu kwa njia ya mazungumzo baina ya Serikali ya Uganda na Waasi wa LRA, lakini pia jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa LRA, inazuiliwa kufanya uhalifu huo uliodumu kwa miaka ishirini na kuhakikisha watu hao wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa sababu endapo haki haitatendeka kundi la LRA na mengine yataendeleza uhalifu huo wa kibinadamu.

Serikali za Sudan, Jamuhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo -DRC kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa zinapaswa kuunganisha nguvu za Kijeshi ili kuweza kuwaokoa mateka hao mapema iwezekanavyo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote waliohusika na utekaji huo.

Mwaka 2005, Viongozi wengi wakuu wa kundi la LRA, walishitakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya makosa ya jinai ya mjini the Hague kutokana na kuhusika katika makosa ya kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.

Kwa mujibu wa Amnesty, kundi la Waasi la LRA, limehamishia mapigano yake Kusini mwa Jamuhuri ya Afrika ya Kati ili kuzuia viongozi wao wasikamatwe na kufikishwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya jinai-ICC.

Mapema mwezi huu mazungumzo ya Amani baina ya Serikali ya Uganda na Kiongozi wa kundi la LRA, Joseph Kony, alishindikana baada ya Kony kushindwa kuhudhuria katika Mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika kwa ajili ya utiaji saini.

Mauaji ya wenyewe kwa wenyewe huko Kaskazini mwa Uganda yameshaua maelfu ya watu na kuwapotezea makazi yao kiasi cha watu zaidi ya milioni mbili.

Mauaji kama hayo pia yamekuwa yakiendelea katika nchi ya Sudan, ambayo ni mzalishaji wa Mafuta na maeneo ya Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yenye utajiri wa madini.

Matumaini ya kumalizika kwa vita hivyo vya muda mrefu yalipotea pale ambapo Kony aliposhindwa kujitoa mafichoni na kushiriki utiwaji saini wa makubaliano ya amani uliotakiwa kufanyika Aprili kumi katika mpaka wa Sudan na Kongo.

Jana, Marekani ilitoa wito kwa kundi la wapiganaji wa chini kwa chini kutia saini makubaliano ya mwisho ya amani, na imeipongeza Serikali ya Uganda kwa kuwa wavumilivu na maamuzi waliyoyachukua wakati wa mazungumzo ya Juba.