Amnesty International yatoa ripoti juu ya majeshi ya serikali ya Sudan
10 Oktoba 2007Ripoti iliyotolewa na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International, imeeleza kwamba eneo la Kaskazini mwa jimbo la Darfur nchini Sudan hali si shwari kwa wananchi kutokana na machafuko ya majeshi ya serikali na yale ya waasi.
Kwa mujibu wa Amnesty International, vikundi vya wanajeshi wa Sudan-Sudan Armed Forces, vimeonekana katika miji sita ya Kaskazini mwa Jimbo la Darfur ambapo miji ya Tine, Kornoy, Um Baru na Kutum, imeonekana na kiasi kikubwa cha askari.
Naibu Mkurugenzi wa shirika hilo kanda ya Afrika Bwana Tawanda Hondora, amesema kutokana na eneo la kaskazini mwa Darfur kuwa chini ya vikosi vya serikali, huenda vinaweza kusababisha mapigano mengine kabla ya mkutano wa amani unaotarajia kufanyika nchini Libya mwishoni mwa mwaka huu.
Ripoti hii ya Amnesty International imetolewa wakati ambapo zaidi ya raia 40 wameuawa katika kipindi kifupi kilichopita baada ya majeshi ya serikali na waasi wa Janjaweed kufanya mashambulizi katika mji wa Muhajeria.
Taarifa imeeleza kwamba mashambulizi hayo yamefanywa na ndege za jeshi la Sudan zikiwa zimepakwa rangi nyeupe kama zile za Umoja wa Mataifa.
Vipande kadhaa vya mabomu na risasi pia vimeonekana karibu na kambi ya Umoja wa Afrika nchini Sudan.
Ofisa wa Shirika la Amnesty International Bwana Hondora amekaririwa akisema kwamba kuwepo kwa majeshi ya serikali ya Sudan katika eneo la kaskazini, mapigano ya Haskanita ya juma lililopita na haya ya hivi punde ni matukio muhimu kwa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kuongeza vikosi vya usalama, ili kulinda maisha ya raia wa Sudan.
‘Wananchi wa eneo hilo wanakabiliwa na hali ya hatari, na Jumuiya ya Kimataifa haipaswi kuchelewa kupeleka msaada wa haraka kwa lengo la kudhibiti vifo vinavyoweza kuzuilika,’ ripoti ya Amnesty International imeeleza.
Katika mashambulizi yaliyofanyika kati ya tarehe tano na sita mwezi huu katika mji wa Haskanita, watu 750 waliyakimbia makazi yao baada ya makazi yao kuungua moto, ambapo ni misikiti na shule pekee vilivyoachwa salama.
Ni katika kipindi hicho pia majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika yalipovamiwa na askari kumi miongoni mwao walipoteza maisha.
Wakati shirika la kutetea haki za binada la Amnesty International likitoa ripoti hiyo, jeshi la Sudan limekanusha kufanya mashambulizi dhidi ya waasi wa Darfur kikundi kilichotia saidi makubaliano na serikali.
Kikundi hicho cha Sudan Liberation Army-SLA ndicho pekee kilichokubali kutia saini makubaliano ya mwaka 2006 kati ya vikundi vitatu vinavyopigana mara kwa mara.
Hata hivyo, kikundi cha waasi wa SLA kimesema wanamgambo wa Janjaweed wanaosaidiwa na serikali bado wanaendeleza machafuko ikiwemo mauaji ya raia na kuchoma nyumba za wananchi.
Kamanda wa kikundi cha waasi wa SLA Bwana Abu Bakr Kadu amesema kuna ndege za serikali zinazowasaidia wanamgambo wa Janjaweed kufanya mapigano katika eneo la kusini mwa Jimbo la Darfur na kuuwa wananchi.