1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty International yamaliza ziara yake Darfur

ELIZABETH KEMUNTO22 Septemba 2004

Ziara iliyofanywa na shirika la kutetea haki za binadamu duniani, Amnesty International, katika eneo la Darfur siku chache zilizopita, imeonyesha ya kwamba Marekani imekuwa dhaifu katika kuingilia kati mizozo inayohusu haki za binadamu katika mataifa mengine.

https://p.dw.com/p/CHiW
Katibu Mkuu wa Amnesty International, Irene Khan, amesema Sudan ni lazima iyakubali makosa yake badala ya kuzungumzia makosa ya Marekani
Katibu Mkuu wa Amnesty International, Irene Khan, amesema Sudan ni lazima iyakubali makosa yake badala ya kuzungumzia makosa ya MarekaniPicha: AP

Kumbu kumbu zinaonyesha kwamba Marekani, ambayo imechukua jukumu la kuhakikisha haki za binadamu zinatekelezwa ulimwenguni, haijaonyesha mfano mzuri katika suala hilo na hasa ikizingatiwa vile visa vya kuwatesa wafungwa wa Abu Ghraib na Guantanamo.

Mkurugenzi mtendaji wa Amnesty International Marekani, amemaliza ziara yake huko Darfur hivi majuzi. Bwana Schulz amesema kwamba Marekani haionwi tena kama mfano mzuri wa uadilifu duniani kwa sababu yenyewe imekosa kutekeleza haki hizo mara kwa mara.

Bwana Schulz amesema kwamba wakati wa mazungumzo na maafisa wa serikali ya Sudan, maafisa hao walitoa mifano ya udhaifu wa Marekani katika kutekeleza haki hizo wanazoitaka Sudan izitekeleza kwa watu wa Darfur.

Schulz aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano huo kwamba, maafisa hao walitumia mifano mibaya iliyotendwa na Marekani, ili kutetea kukosa kwao kuchukua hatua dhidi ya uhalifu uliofanywa huko Darfur. Lakini tukio hilo linaonyesha kwamba Marekani haina haki ya kushutumu nchi zingine kama yenyewe inatenda maovu dhidi ya haki za binadamu.

Maafisa wa Sudan walizungumzia mifano ya wafungwa wa Abu Ghraib mjini Baghdad na mateka wa vita wa Guantanamo Bay ambao wameteswa chini ya utawala wa Marekani.

Marekani sasa inahitaji kufanya zaidi ya kupitisha maazimio tu na kutishia kuweka vikwazo ikiwa inataka matokeo yoyote yatakayoleta mabadiliko.

Lakini hii sio mara ya kwanza kwa Marekani kupatikana upande wa makosa katika suala la haki za binadamu. Katibu mkuu wa Amnesty International, Irene Khan, amesema shirika hilo na mashirika mengine ya haki za binadamu yamekabiliwa na wakati mgumu katika kazi yao, tangu kuanza kwa kile Marekani inachokiita vita dhidi ya ugaidi. Hii ni kwa sababu vita hivyo vinakiuka haki za raia.

Bi Khan aliongeza kwamba Sudan sio nchi ya kwanza kulalamika kuhusu historia ya Marekani ya kukiuka haki za binadamu, kwani nchi zingine barani Afrika na Asia pia zimetoa malalamisha kama hayo.

Kwa upande mwingine, sio Marekani tu ambayo inafanya unafiki kuhusu suala la haki za binadamu. Lakini Bi Khan amesema ingawa Sudan inatafuta njia rahisi ya kuepuka makosa yake kwa kuilaumu Marekani, ni lazima iuchukue mzigo wake yenyewe.

Ujumbe wa Amnesty International uliokwenda Darfur, umesema uliwaona watu ambao maisha yao yalikuwa yameharibiwa, serikali ambayo ilikuwa inakanusha madai ya kuhusika katika mzozo nchini humo na watu wengi wamekufa moyo kwa sababu hatua za kutatua mzozo huo zinachukua muda mrefu kutekelezwa.

Bi Khan ameeleza kwamba huenda hali ikawa mbaya zaidi katika kambi za wakimbizi kwani sasa wakimbizi hao wanapata asilimia arobaini na tano tu ya chakula ambacho wanakihitaji. Tatizo kubwa nchini Sudan ni mawasiliano, kwani bara bara ni mbovu na hivyo kusafirisha chakula cha kuwalisha zaidi ya watu milioni moja sio jambo rahisi.

Kuna hali ya wasiwasi katika kambi za wakimbizi. Watu hawakubaliwi kutoka nje ya kambi zao na baadhi ya watu hawafurahii kufungiwa. Baadhi yao wamewavamia wafanya kazi wa mashirika ya misaada.

Makundi ya watu wanaohama hama na mifugo yao, tayari yameshaanza kukalia makazi ya watu waliohama kwa hofu ya kuvamiwa, na kusababisha hali ya mvutano. Mvutano huu huenda ukalipuka na kuwa mzozo mkubwa kwani bado wanawake wanabakwa na watu wanalazimishwa kuyahama makazi yao.

Serikali ya Sudan ilionyesha kwa njia ya televisheni baadhi ya hatua ambazo imechukua dhidi ya wale waliofanya uhalifu huko Darfur, lakini baadaye ikadhihirika kwamba hatua hizo zilikuwa dhidi ya uhalifu wa kawaida kama vile utumizi mbaya wa fedha.

Habari zingine zinasema kwamba wanamgambo wa Janjaweed ambao wanatuhumiwa kwa maovu yaliyofanyika huko Darfur, sasa wanafanya kazi kama walinzi katika makambi ya wakimbizi. Hayo yalisemwa na kamishna mkuu wa Shirika la kuwahudumia wakimbizi duniani (UNHCR), LOUISE ARBOUR, baada ya kutembelea eneo la Darfur. Arbour amesema aliambiwa na wakimbizi katika makambi kaskazini mwa Darfur kwamba maadui wao ndio sasa wamejiunga na kikosi cha polisi na ndio walinzi wao katika makambi hayo.