1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AMISOM yauwa raia wawili Somalia

Aboubakary Jumaa Liongo24 Novemba 2010

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia, AMISOM, jana kililazimika kulifyatulia risasi kundi la raia na kuwaua raia wawili katika mji mkuu, Mogadishu.

https://p.dw.com/p/QGpF
Picha: Daniel Scheschkewitz

Kufuatia tukio hilo, AMISOM imetoa taarifa ya kuomba radhi.

Katika taarifa yake, AMISOM imesema uchunguzi kufuatia tukio hilo unaendelea, lakini taarifa walizonazo mpaka sasa ni kwamba msafara wa kikosi hicho, uliyokuwa ukitoka katika kambi yake, ulifyatua risasi kwa bahati mbaya dhidi ya kundi la raia karibu na eneo la Umoja wa Mataifa. Limesema mmoja wa watu waliyojeruhiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya jeshi hilo.

Kamanda wa kikosi hicho cha Afrika nchini Somalia, Meja Jenerali Nathan Mugisha, amesema mpaka sasa hawajafahamu iwapo wanajeshi walifyatua risasi katika hali ya kujihami, lakini, hata hivyo, askari wote waliyohusika wamekamatwa, wakati uchunguzi kamili ukiendelea.

Kikosi hicho cha Afrika nchini Somalia kina wanajeshi 7,500 kutoka Uganda na Burundi, ambacho kinaisadia serikali ya mpito nchini humo kukabiliana na makundi ya wanamgambo wa kiislam.