1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amerika ya Kusini sasa yaongoza kwa maambukizi ya corona

Zainab Aziz Mhariri: Zingo babu Abdallah
23 Mei 2020

Shirika la afya duniani WHO limesema kitovu cha maambukizi ya virusi vya corona sasa kipo katika nchi za Amerika Kusini baada ya takwimu kuonyesha kuna kasi kubwa ya maambukizi ya virusi hivyo katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/3cfnB
Brasilien Intensivstadion COVID-19 Sao Paulo | José Wilke
Picha: DW/G. Basso

Kutokana na kulipuka kwa maambukizi zaidi kwenye nchi za Amerika Kusini na ya kati, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona duniani kote sasa inakaribia milioni 5.2 na watu zaidi ya 337,000 wameshakufa. Nchini Brazil pekee idadi ya watu waliokufa imepindukia watu 20,000. Watu wengine 310,000 wameambukizwa nchini humo. Sasa nchi hiyo inashika nafasi ya tatu duniani kwa maambukizi, ikizifuatia Marekani na Urusi.

Mkururugenzi wa kitengo cha hali ya dharura kwenye shirika la afya duniani Mike Ryan amethibitisha kwamba Amerika ya Kusini sasa imekuwa kitovu cha maradhi ya Covid -19. Ameeleza kuwa wameshuhudia kuongezeka kwa maambukizi katika nchi nyingi za Amerika Kusini, hata hivyo amesema Brazil ndiyo iliyoathirika zaidi kwa sasa.

Rais wa Brazil Jair Bolsonaro
Rais wa Brazil Jair BolsonaroPicha: AFP/E. SA

Tofauti na barani Ulaya na Marekani ambako wazee ndiyo walioathirika zaidi, nchini Brazili idadi kubwa ya  watu waliokufa walikuwa vijana waliojikuta katika hali ya kulazimika kufanya kazi licha ya hatari ya maambukizi. Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza kutoka chuo kikuu cha Brasilia Mauro Sanchez amesema watu wengi wanajiweka katika hatari ya kupata maambukizi kwa sababu hawana njia nyingine. Wachimba makaburi katika mji wa Sao Paulo wamesema wanalemewa na kazi ya kuzika kutokana na idadi kubwa ya vifo.

Wakati huo huo nchini Marekani rais Donald Trump anayedhamiria kutafuta njia ya kuondokana na mgogoro wakati ambapo anakabiliwa na changamoto ya kutaka kuchaguliwa tena, ameongeza shinikizo kwa serikali za majimbo na za mitaa ili kulegeza hatua za karantini. Janga la corona limeuathiri uchumi wa Marekani kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba miito inatolewa juu ya kulegeza hatua hizo licha ya kuongezeka kwa maambukizi. Watu zaidi ya Milioni 1.6 wameambukizwa virusi vya corona nchini humo na zaidi ya watu 96,000 wameshakufa.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: picture-alliance/AP/A. Brandon

Rais Trump amewataka magavana wa majimbo wazipe umuhimu sehemu za ibada sawa na huduma muhimu kama vile chakula na maduka ya dawa. Ameruhusu ibada kufanyika licha ya kuzuia mikusanyiko ya hadhara. Trump amesema magavana wanapaswa kuchukua hatua sahihi kwa kuruhusu mara moja nyumba za ibada kufunguliwa. Rais Trump anawelenga waumini anaowazingatia kuwa ngome muhimu katika uchaguzi mkuu ujao. Rais huyo amesema Marekani inahitaji maombi kwa mungu na ameeleza kuwa ikiwa magavana hawataruhusu atatumia turufu kuwapiku.

Hata hivyo wataalamu wametahadharisha kwa kueleza kuwa bila ya kupatikana chanjo, hatua za karantini zinapaswa kuendelezwa lakini hali hiyo inaathiri shughuli za kiuchumi. Wataalamu hao wametahadharisha juu ya hatari ya kuzuka wimbi jingine la maambukizi nchini Marekani.

Wakati huo huo Urusi imeripoti vifo vya watu 3,249 na kuongezeka kwa watu zaidi ya 325,000 walioambukizwa virusi vya corona nchini humo. Meya wa mji wa Moscow, Sergei Sobyanin amesema idadi ya wagonjwa mahututi inaongezeka kiasi kwamba madaktari wanapaswa kuwachagua watakaotibiwa na watakaoachwa bila ya matibabu. Meya huyo amekiri kwamba haiwezekani kuyaokoa maisha ya watu wote.!  

Vyanzo: AFP/APE