Amazons: Kikosi cha wanawake cha Dahomey
26 Februari 2021Dahomey eneo linalojulikana leo hii kama Benin lilikuwa ni moja wapo ya falme za kale za Kiafrika. Wafalme kumi na tano tofauti walitawala eneo hilo, lakini hakuna rekodi za kumbukumbu zinazotaja majina ya wanawake wa ufalme huo. Hata hivyo, wanawake walichangia kuuimarisha ufalme huo, na mwanamke mmoja aliwahi hata kutawala.
Nani alikuwa mpiganaji wa kwanza wa kikosi cha Dahomey Amazon?
Kulingana na mwanahistoria Bienvenu Akoha, mpiganaji wa kwanza wa Amazons alikuwa ni Tassi Hangbe, mtoto wa Mfalme Houegbadja, mwasisi wa ufalme wa Dahomey, na pacha wa Mfalme Akaba. Mnamo mwaka 1708 mfalme Akaba alifariki baada ya kuugua kwa muda mrefu. Tassi Hangbe akateuliwa kama mkuu wa jeshi. Baada ya hapo aliondoka na kwenda kupigana vita. Aliporudi vitani, ndipo akatangazwa rasmi kama Malkia wa Dahomey.
Tassi Hangbe alileta mafanikio gani wakati wa utawala wake?
Licha ya kwamba alitawala kwa miaka mitatu pekee, Tassi Hangbe alifanya mengi kuwainua wanawake. Aliwapa jukumu la kuwinda na kutunza mashamba. Kabla ya hapo, kazi zote hizo mbili zilizoeleka kufanywa na wanaume. Pia aliendeleza kilimo, na kusambaza maji ya kunywa bure kwa watu wake wote.
Wanawake wa Dahomey Amazons walijitofautishaje?
Mara tu baada ya kutawazwa, Tassi Hangbe alihisi kuwa hataweza kufanya kila anachotaka, kwa hivyo aliunda kikosi cha wanawake watupu waliokuwa na ushujaa wa hali ya juu. Wapiganaji hao waliojulikana pia kama Agoodjie kwa lugha ya Fon (jina linalomaanisha kikosi cha mwisho cha ulinzi kabla ya kumfikia malkia), walianza kupewa mafunzo tangu wakiwa watoto. Na mafunzo hayo yaliyokuwa na ufanisi mkubwa, yaliwajenga na kuwa wapiganaji mashujaa kuliko wanaume wengi. Wakiwa vitani, wanawake hao huwa hawana huruma. Na anaethubutu kutaka kuwapinga alikatwa kichwa.
Miongo michache kufuatia utawala wa Tassi Hangbe, alitawazwa Mfalme Guézo. Na alikifufua kikosi cha Amazons kikiongozwa na jemedari Seh Dong Hong Beh (Sê do Houngbé kwa lugha ya Fon). Kazi kuu ya kikosi hicho ilikuwa ni kumkamatia mateka waliouzwa kama watumwa kwa mfanyabiashara ya utumwa kutoka Brazil. Na badala yake, mfanyabiashara huyo akimletea mfalme Guézo bunduki, poda ya bunduki, tumbaku, na pombe.
Kikosi cha Dahomey Amazons kinakumbukwaje?
Mwaka 1882, Mfalme Behanzin, alitaka kulinda haki yake ya kibiashara. Na hivyo akapigana vita na wakoloni wa Ufaransa. Lakini jeshi la Ufaransa lilikuwa limejizatiti vilivyo kwa silaha, na kukishinda vibaya kikosi cha Amazons. Licha ya kutenda kile ambacho leo hii kingeangaliwa kama uhalifu wa kivita, kikosi cha Amazons kinasifiwa kwa kumkomboa mwanamke wa Kiafrika. Baada ya mchango wao kihistoria kupuuzwa kwa miaka mingi, hivi sasa pole pole mashujaa hao wa kike wanaanzwa kukumbukwa kwa hadhi inayowastahili. Huko Abomey, makumbusho ya Tassi Hangbe imenaza kujengwa. Mbali na hilo, jamaa zake huwa wanamfanyia sherehe maalumu zinazojumuisha kuimba na kucheza.
Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.