1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aliyetibua njama ya Al Qaeda ni mfanyikazi wa shirika la kijasusi la CIA

MjahidA9 Mei 2012

Mwanamume aliyechaguliwa na kundi la kigaidi la Alqaeda nchini Yemen kutekeleza njama ya kuripua ndege ya Marekani imegunduliwa ni mfanyikazi katika shirika la kijasusi la Marekani CIA.

https://p.dw.com/p/14sAn
Nembo ya shirika la kijasusi la Marekani CIA
Nembo ya shirika la kijasusi la Marekani CIAPicha: picture-alliance/Landov

Kulingana na vyombo vya habari nchini Marekani mwanamume huyo alitakiwa kuripua ndege kwa kutumia bomu lililokuwa limeshonwa ndani ya chupi.

Marekani imesema mtu aliyetumwa na kundi hilo la kigaidi kuripua bomu katika moja ya ndege zake, ni mfanyikazi wa shirika la kijasusi la nchi hiyo na pia shirika la kijasusi la Saudi Arabia na kwamba kwa sasa ameshaondoka nchini Yemen.

Hata hivyo Mtu huyo hakutekeleza azma ya Alqaeda ya kuliripua bomu hilo ndani ya ndege ya Marekani badala yake moja kwa moja alikipeleka kifaa hicho cha mripuko kwa serikali ya Marekani hatua iliyorudisha nyuma njama hizo za kigaidi.

Mtaalamu wa maswala ya usalama nchini Marekani Richard A.Clarke
Mtaalamu wa maswala ya usalama nchini Marekani Richard A.ClarkePicha: ITAA

Richard Clarke mtaalamu wa maswala ya Usalama nchini humo amesema, kwa kupata bomu hilo sasa wataalamu watakuwa na uwezo wa kugundua namna linavyofanya kazi na namna ya kugundua mabomu mengine ya aina hiyo.

Kwa sasa bado shirika la upelelezi la Marekani linafanyia uchunguzi bomu hilo lakini maafisa nchini humo wanasema bomu lililopatikana lilikuwa la hali ya juu mno kuliko lile la mwaka wa 2009. Maafisa hao wameongeza kuwa wanaamini mfumo wa usalama uliowekwa katika viwanja vya ndege nchini Marekani katika miaka ya hivi karibuni ungeweza kugundua aina ya bomu lililopatikana.

Jaribio la awali

Aliyejaribu kuripua ndege ya Marekani mwaka wa 2009, Umar Farouk Abdulmutallab
Aliyejaribu kuripua ndege ya Marekani mwaka wa 2009, Umar Farouk AbdulmutallabPicha: AP

Itakumbukwa kwamba mwaka 2009 njama kama hiyo ilishindikana baada ya bomu lililokuwa limeshonwa ndani ya chupi ya mwanamume mmoja raia wa Nigeria Umar Farouk Abdulmutallab, kushindwa kujiripua mjini Detroit Marekani, kisha ikatokea njama nyingine ya wanaojitoa mhanga kuficha mabomu katika kifaa cha uchapishaji yani printer na kugundulika katika ndege ya mizigo mwaka wa 2010, utawala wa Marekani ulifanikiwa kuzima njama hizo.

Sasa Marekani inaamini kwamba bomu hili lililogunduliwa limetengenezwa na mtaalamu wa kutenegeneza mabomu wa kundi la Al Qaeda Ibrahim Hassan al-Asiri ama moja ya wanafunzi wake.

Hata hivyo Waziri wa ulinzi Leon Edward Panetta, amesema, Marekani inastahili kuwa chonjo dhidi ya walio na nia ya kushambulia nchi hiyo na kwamba maafisa wa usalama watafanya kila wawezalo kuilinda Marekani.

Mwandishi Amina Abubakar/AP

Mhariri Yusuf Saumu