1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchunguzi wa vita vya Irak.

Abdu Said Mtullya12 Januari 2010

Aliekuwa afisa wa karibu wa Tony Blair asema, waziri Mkuu huyo alitaka kuondolewa kwa silaha za Saddam Hussein nchini Irak, na siyo kuuangusha utawala wake.

https://p.dw.com/p/LToO
Aliekuwa waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair atarajiwa kutoa ushahidi juu ya vita vya Irak siku zijazo .Picha: AP

Mkurugenzi wa habari wa waziri mkuu wa Uingereza wa hapo awali leo amesema kwamba yeye hakuwa na uzito wa mbele katika kupitisha sera juu ya Uingereza kuivamia Irak.

Mkurugenzi huyo wa zamani, Alistair Campbell, alisema hayo kwenye jopo linalofanya uchunguzi juu ya kuhusika kwa Uingereza katika vita vya Irak.

Alistair Campell,aliekuwa mkurugenzi wa habari wa waziri mku Tony Blair, aliliambia jopo hilo kwamba alihudhuria mikutano mingi muhimu, lakini hakuunda sera.

Bwana Campbell aliulizwa maswali na wanajopo wanaofanya uchunguzi wa vita vya Irak juu ya dhima aliyokuwa nayo katika kutayarisha nyaraka za utatanishi.

Katika nyaraka hizo za mwaka 2002 , serikali ya waziri mkuu Tony Blair ilidai kwamba palikuwa na uwezekano wa Saddam Hussein kuwa na silaha za maangamizi. Sababu iliyoifanya Uingereza isimame pamoja na Marekani katika kuivamia Irak.

Hata hivyo, bwana Campbell amewaambia wanajopo wa uchunguzi kwamba hapakuwa na papara za kuingia katika vita, licha ya uhusiano wa ndani baina ya aliekuwa waziri mkuu wa Uingereza, Tony Blair, na rais wa Marekani wa hapo awali, George Bush.Campbell amesema kuwa waziri mkuu Blair alijaribu kutafuta suluhisho la amani kabla ya kuivamia Irak mnamo mwaka 2003.

Aliliambia jopo la uchunguzi kwamba siyo kama watu wanavyofikiria kuwa waziri mkuu Blair alitaka tu kuivamia Irak na kumng'oa Saddam Hussein bila ya kujali hoja za ukweli. Bwana Campbell amesema waziri mkuu Blair wakati huo alikuwa na wasiwasi juu ya mwambatano uliokuwapo kati ya silaha za maangamizi, serikali za kikorofi na ugaidi, na kwamba wasiwasi huo ulikuwapo hata kabla ya kufanyika mashambulio ya tarehe 11 mwezi septemba mwaka 2001 nchini Marekani.

Hatahivyo amesema waziri mkuu Blair alikuwa anatafuta njia ya kupunguza silaha nchini Irak wakati rais Bush alikuwa analenga shabaha ya kumng'oa Saddam Hussein.

Uchunguzi juu ya vita vya Irak unafanywa na jopo la watu watano kwa lengo la kujifunza kutokana na vita hivyo.Aliekuwa waziri mkuu wa wakati huo bwana Blair atafika mbele ya jopo hilo mnamo wiki zijazo.

Uchunguzi huo unafanyika wakati nyeti katika siasa za nchini Uingereza.Uchaguzi unatarajiwa kufanyika mnamo mwezi juni ambapo wahafidhina, wanabashiriwa kuwa watashinda.

Wanachama wengi wa chama cha leba bado wamemkasirikia Tony Blair kwa kuitumbukiza Uingereza vitani ambapo askari 179 wa nchi hiyo waliuawa nchini Irak.

Bwana Campbell pia amesema leo kwamba waziri mkuu wa sasa GordonBrown ,ambae alikuwa waziri wa fedha chini ya Blair alikuwa miongoni mwa washauri wa ndani wa waziri mkuu Blair.

Mwandishi: Abdu Mtullya/AFP

Mhariri: Miraji Othman