ALGIERS: Watu wanane wauwawa kwenye mlipuko wa bomu
11 Julai 2007Watu wanane wameuwawa kwenye mlipuko wa bomu uliotokea karibu na kambi ya jeshi la Algeria katika kijiji cha Lakhdaria yapata kilomita 120 mashariki mwa mji mkuu Algiers.
Duru za usalama zimeripoti kwamba watu kadhaa wamejeruhiwa kwenye mlipuko huo.
Usalama umeimarishwa huku mashindano ya michezo ya All Africa Games yatakayojumulisha wanariadha 8,000 kutoka nchi zaidi ya 20, yakitarajiwa kufunguliwa rasmi nchini Algeria.
Kufikia sasa hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na shambulio hilo. Kundi la waasi la Salaf lenye mafungamano na kundi la kigaidi la Al- Qaeda limekuwa likidai kuhusika na mashambulio kama hayo.
Watu takriban laki mbili wameuwawa katika umwagaji damu wa kisiasa nchini Algeria tangu mwaka wa 1992 wakati wafuasi wa chama chenye itikadi kali ya kiislamu kilipoanzisha mapambano ya upinzani.
Chama hicho kilianza mapigano hayo kilipopigwa marufuku wakati kilipokaribia kushinda uchaguzi nchini Algeria.