1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ALGIERS : Waarabu wazinduwa upya mpango wa amani kwa ardhi

24 Machi 2005
https://p.dw.com/p/CFU6

Viongozi wa Kiarabu hapo jana wamekubali kurudisha uhusiano wa kawaida na Israel ili nchi hiyo nayo iondoke katika ardhi ilizoziteka katika vita vya mwaka 1967 sharti ambalo Israel imekuwa ikilikataa mara kwa mara.

Taarifa iliosomwa wakati wa kikao cha mwisho cha mkutano wa viongozi wa Umoja wa Waarabu mjini Algiers Algeria imesema amani ni chaguo muhimu kwa mataifa ya Kiarabu kusuluhisha mzozo wao na taifa hilo la Kiyahudi.

Pendekezo hilo la kubadilishana amani kwa ardhi ni uzinduzi mpya wa mpango wa amani mwa mwaka 2002.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Israel Ariel Sharon amefuta uwezekano wa kufikia muafaka juu ya maeneo inayoyakalia kwa mabavu ya Jerusalem ya Mashariki na Milima ya Golan.

Radio ya Israel imeripoti kwamba wakati wa mkutano na wanachama wa msimamo mkali wa chama chake mwenyewe cha Likud Sharon amesema kwamba hawatoondoka Jerusalem ya Mashariki ambayo ni maakazi ya Wapalestina 200,000 au Milima ya Golan iliokuwa ya Syria maeneo ambayo yote imeyateka wakati wa Vita vya mwaka 1967 kati ya Israel na Waarabu.