Algiers. Gadafi awaita Waisrael na Wapalestina wajinga.
23 Machi 2005Kiongozi wa Libya kanali Muammar Gadafi ambaye hatabiriki kwa kauli zake, amewaacha hoi viongozi wenzake wa mataifa ya Kiarabu pale alipowaelezea Waisrael na Wapalestina kuwa ni watu wajinga. Aliyasema hayo katika kikao cha mwisho cha jumuiya ya Kiarabu kinachofanyika katika mji mkuu wa Algeria , Algiers. Amesema kuwa Waisrael wanakufa kwa wingi kwa sababu wanalikalia kinyume na sheria eneo la ukingo wa magharibi na ukanda wa Gaza. Akaongeza kuwa kama maeneo haya ni muhimu sana kwa Waisrael kwa nini wasiyachukue mapema, na badala yake wakakamata ardhi nyingine za Waarabu. Bwana gadafi pia amesema kuwa Wapalestina pia ni wajinga kwa kuwa wamepoteza maeneo yao katika vita ya mwaka 1967.
Viongozi hao ikiwa ni pamoja na rais wa Palestina, Mahmoud Abbas ambaye ndio mara yake ya kwanza kuhudhuria kikao hicho kama rais baada ya kifo cha Yasser Arafat, mwezi Novemba mwaka jana , nae alikuwa hoi kwa kicheko. Bwana Gadafi ambaye hadi hivi karibuni alikuwa ametengwa na mataifa ya magharibi , aliitetea Syria kwa kujitolea mhanga kwa mambo mengi nchini Lebanon , na kusema kuwa amekasirishwa na hatua ya jumuiya ya kimataifa kuilazimisha kuondoa majeshi yake kutoka Lebanon.