1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Albright asisitiza umuhimu wa uhusiano wa Marekani na Ulaya

7 Novemba 2013

Shughuli za upelelezi zilizofanywa na Shirika la Marekani la Usalama wa Taifa-NSA, zimesababisha kuvunjika kwa hali ya kuamiana baina ya Marekani na nchi za Ulaya.

https://p.dw.com/p/1ADT8
Waziri wa Zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Madeleine Albright
Waziri wa Zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Madeleine AlbrightPicha: picture-alliance/AP/CBS

Hali hiyo ya kuaminiana tena baina ya pande hizo mbili, itawezaje kujengwa upya? Watu mashuhuri nchini Marekani ikiwa pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Madeleine Albright wanaamini kwamba rafiki wa kweli wanaweza kupatana tena baada ya kukosana.

Akizungumza katika mahojiano na ripota wa DW mjini Washington juu ya mvutano uliopo sasa baina ya Marekani na nchi za Ulaya, Albright amesema hilo ni jambo la kusikitisha sana. Zaidi anafafanua, ''Mimi wakati wote nimekuwa muungaji mkono mkubwa wa uhusiano baina ya Marekani na nchi za Ulaya. Sisi ni washirika wa asili. Tunahitajiana. Na kwa hivyo ninayo imani, kwamba mawasiliano na mfungamano utarejeshwa tena.Kimsingi historia yetu ni ya kuaminiana na ndiyo sababu ninayo matumaini."

Mvutano baina ya Marekani na nchi za Ulaya

Katika muktadha wa mvutano baina ya Marekani na nchi za Ulaya uliosababishwa na upelelezi uliofanywa na shirika la Marekani la NSA, aliyekuwa balozi wa Ujerumani nchini Marekani, Wolfgang Ischinger aliwaalika watu mashuhuri kutoa maoni yao.

Balozi wa zamani wa Ujerumani nchini Marekani, Wofgang Ischinger
Balozi wa zamani wa Ujerumani nchini Marekani, Wofgang IschingerPicha: dapd

Walioalikwa ni pamoja na aliyekuwa mgombea wa urais wa Marekani, seneta wa chama cha Republican, John McCain na Bibi Albright.

Waziri huyo wa zamani amesema alipokuwa kazini hakujua chochote juu ya shughuli hizo za upelelezi. Lakini ameeleza kuwa inapaswa kutambua kwamba nchi zinapelelezana. ''Hilo si jambo jipya. Pande zote zinafanya upelelezi."

Aidha, mwandishi wa DW alitaka kujua iwapo Bibi Albright anafahamu kiwango cha gadhabu barani Ulaya juu ya utawala wa Obama. Akilijibu swali hilo Bibi Albright ameeleza. ''Hapana, kwa kweli sielewi. Kwa sasa mambo mengi yana sababu za kisiasa.''

Akifafanua zaidi anasema, ''naamini, kwa kiwango kikubwa hayo yanatokana na tekinolojia za kisasa. Hilo ni tatizo la jumla. Sasa inatupasa sote kwa pamoja tuzifafanue kanuni za medani ya faragha katika enzi hizi za tekinolojia za kisasa. Natumai tutalijadili suala hilo kwa makini na kupata ufumbuzi.''

Seneta John McCain
Seneta John McCainPicha: imago/UPI Photo

Matatizo yanazikabili Marekani na nchi za Ulaya

Waziri wa mambo ya nje wa zamani wa Marekani Madeleine Albright amesema Marekani na nchi za Ulaya zinakabiliwa na matatizo mengi na hivyo zinapaswa kushirikiana.

Amesema Marekani na nchi za Ulaya zina ajenda kubwa ya pamoja. Lakini ukweli unahitajika kutoka kila upande. Bibi Albright ameshauri kufanyika kwa mjadala kwa kuuzingatia moyo wa kuelewana.Ameeleza kuwa kimsingi Marekani na nchi za Ulaya ni rafiki wa dhati.

Kutokana na hayo ameshauri kuendelea kutekelezwa kwa mapatano yote yaliyofikiwa baina ya Ulaya na Marekani juu ya masuala muhimu ikiwa ni pamoja na makubaliano kuhusu kubadilishana data muhimu yanayohusu mambo ya usalama na benki. Pia ameshauri kuendelezwa kwa mazungumzo baina ya Marekani na Umoja wa Ulaya juu ya kuunda ukanda wa biashara huru.

Mwandishi: Schließ,Gero
Tafsiri: Mtullya Abdu.
Mhariri: Josephat Charo