1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Zawahiri amrithi Bin Laden

16 Juni 2011

Mtandao wa Al-Qaida umemtaja daktari wa Kimisri, Ayman Al-Zawahiri, kuwa mrithi wa Osama bin Laden na tayari Zawahiri ametangaza vita vitakatifu dhidi ya taifa la Marekani na mshirika wake mkuu, Israel.

https://p.dw.com/p/11cDR
Ayman Al-Zawahiri, kiongozi mpya wa Al-Qaida
Ayman Al-Zawahiri, kiongozi mpya wa Al-QaidaPicha: youtube.com

Mwanamme huyu anayefuga ndevu wa miaka 59 na anayevaa kilemba cheupe kila anapoonekana, amekuwa kiini cha uongozi wa kisiasa wa Al-Qaida kwa muda mrefu. Mtandao wa Al-Qaida umemtangaza rasmi sasa kuwa kiongozi wake, kuchukuwa nafasi ya Bin Laden aliyeuawa na majeshi ya Marekani mwanzoni mwa mwezi uliopita.

Guido Steinberg, mtaalamu wa masuala ya Kiislam katika taasisi ya Sayansi ya Siasa hapa Ujerumani, anasema kuwa Ayman Al-Zawahiri alikuwa ni kiongozi namba mbili wa mtandao huu, na isingeliwezekana kwa mwengine asiyekuwa yeye "kuchukua nafasi hii ya uongozi wa Al-Qaida."

Zawahiri alizaliwa mwaka 1951 katika mtaa wa Maadi kwenye mji mkuu wa Misri, Cairo. Baba yake alikuwa ni daktari, na ami yake alikuwa ni imamu katika Chuo Kikuu kinachoheshimika cha Al-Azhar.

Tangu utotoni, Ayman alionekana kufuata nyayo za baba yake na akasomea udaktari jijini Cairo. Akiwa kijana, alikuwa mwanachama wa kundi la Ikhwanul-Muslimina, ambalo baadaye lilikuja kupigwa marufuku na serikali. Baada ya kumaliza masomo yake, alijiunga na jeshi la nchi yake, kama daktari wa upasuaji, na baadaye akafanya kazi kama daktari wa kawaida jijini Cairo.

Osama bin Laden (kushoto) na Ayman al-Zawahiri
Osama bin Laden (kushoto) na Ayman al-ZawahiriPicha: AP

Kufuatia kuuawa kwa Rais Anwar Saadat hapo mwaka 1981, Ayman alikamatwa na kuwekwa jela kwa miaka mitatu, akishukiwa kuhusika na mauaji hayo.

Baada ya kuachiwa huru, alisafiri kwenda Afghanistan kupigana vita vitakatifu dhidi ya vikosi vya lililokuwa Shirikisho la Kisovieti nchini humo. Ni hapo ndipo alipokutana na Osama bin Laden.

Baada ya vita hivi kumalizika, Zawahiri alifufua upya vita vyake dhidi ya serikali ya Misri. Mwaka 1995 kulifanyika jaribio la mauaji dhidi ya rais wa wakati huo wa Misri, Hosni Mubarak, mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambalo linasemekana kupangwa na Zawahiri.

Mwaka 1998, mahakama nchini Misri ilimuhukumu kifo, bila ya yeye mwenyewe kuwapo. Hadi hapo tayari, Zawahiri alishakuwa sehemu muhimu ya mashambulizi ya kigaidi.

Guido Steinberg anasema kwamba hili linamaanisha kuwa Zawahiri alikuwa ni mtu aliyejengeka kisiasa. "Lengo lake lilikuwa na limeendelea kuwa na dola ya Kiislamu nchini Misri. Vijana wengi wa Al-Qaida hawana malengo ya kisiasa kama yeye. Daima Zawahiri amekuwa ndiye mpangaji mikakati mkuu wa mtandao huu na alisimama kama nguzo imara kwa Osama bin Laden."

Mwaka 1988 Osama bin Laden alianzisha mtandao wa Al-Qaida, ambao katika miaka 90 ukaja ukawa kiungo cha mitandao kadhaa ya Waislamu wenye siasa kali ulimwenguni.

Yeye na Zawahiri wakashirikiana katika mipango ya mashambulizi dhidi ya balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania hapo mwaka 1998.

Mashambulizi haya ulikuwa ni ushindi mkubwa kwa ushirikiano wa watu hawa wawili, ambao uliwahamasisha kupanga na kufanya mashambulizi mengine ndani ya ardhi ya Marekani hapo Septemba 11, 2001.

Katika miaka ya mwisho, mara zote Bin Laden na Zawahiri walionekana pamoja kwenye mikanda ya video, inayoelezea dhana yao ya mapambano.

Tangu wakati huo, Zawahiri amekuwa akidai kuhusika kwa njia moja ama nyengine na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Marekani, iwe nchini Afghanistan au Iraq. Hata katika mashambulizi dhidi ya raia yaliyofanyika kwenye treni ya chini ya ardhi, nchini Uingereza hapo mwaka 2005.

Wakati huo, Zawahizi alisema kwamba Al-Qaida ilifanya mashambulizi hayo ya London, "ikiwa ni kulipiza kisasi kiburi cha Uingereza na ukandamizaji wa vita vya msalaba vya Marekani ambavyo vimefanywa dhidi ya mataifa ya Kiislamu kwa miaka 100 sasa."

Baada ya kifo cha Bin Laden, jina la Zawahiri limepanda na kuwa la kwanza katika orodha ya Idara ya Upelelezi ya Marekani, FBI. Pamoja na viongozi wengine wa Al-Qaida, Zawahiri amekuwa kiini cha mashambulizi ya Taliban nchini Pakistan.

Hata hivyo ameweza kunusurika majaribio kadhaa ya kumuua kutoka jeshi la Marekani.

Kuchukuwa kwake uongozi wa Al-Qaida kunaweza kuwa mwanzo mpya wa mashambulizi ya mtandao huo wa kigaidi, lakini kuna ukweli kwamba kwa siku za karibuni, Al-Qaida yenyewe imekuwa haina nguvu tena ilizokuwa nazo mwishoni mwa miaka ya '90 na mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Mwandishi: Daniel Scheschkewitz/DW
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Saumu Mwasimba