Al-Sissi anasema lazima IS ikabiliwe kwa pamoja
17 Februari 2015Wito huo wa rais al-Sissi kwa Umoja wa Mataifa umetolewa katika mahojiano na kituo cha Redio cha Europe 1 cha nchini Ufaransa, ambayo yamerushwa hewani leo Jumanne. Kiongozi huyo amesema na hapa namnukuu, ''Hakuna chaguo jingine, tukitilia maanani ridhaa ya watu wa Libya na serikali yao, ambao wanatutaka kuchukua hatua'', mwisho wa kumnukuu.
Hayo yanajiri baada ya Misri kuvishambulia kwa ndege vituo vya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS nchini Libya, kufuatia mauaji ya yaliyofanywa na kundi hilo dhidi ya raia 21 wa Misri wa madhehebu ya Koptiki. IS ambayo tayari inashikilia maeneo makubwa ndani ya Syria na Iraq, ilikuwa imetoa mkanda siku ya Jumapili, unaoonyesha wakristo hao wa Misri wakichinjwa mmoja baada ya mwingine.
Wakoptiki walaani ''Bahari ya Damu''
Jamii ya wakoptiki jana ilifanya maandamano kuonyesha kukerwa na vitendo hivyo vya mauaji dhidi ya wenzao, na waliunga mkono mashambulizi ya kulipiza kisasi.
''Mashambulizi yaliyoidhinishwa na rais al-Sissi ndio pekee yaliyotutuliza mioyo. Usiku wa jana hatukupata usingizi kutokana na picha za kutisha za umwagaji damu. Tuliona bahari ya damu, ulimwengu mzima uliiona bahari hiyo ya damu.'' Alisema mwandamanaji huyo wa kikoptiki.
Rais al-Sissi alipoulizwa kama mashambulizi hayo yaliyoanza jana yangeendelea, alisema hawana budi kuyaendeleza, akiongeza kuwa hatua hizo yabidi zichukuliwe kwa pamoja.
Operesheni ambayo haijahitimishwa
Akirejelea vita vya mwaka 2011 nchini Libya ambavyo viliishirikisha Ufaransa katika muungano uliowasaidia wapinzani dhidi ya kiongozi wa wakati huo Muammar Gaddafi, rais al-Sissi aliviita vita hivyo ''Operesheni ambayo bado haijakamilika''.
''Tuliwaacha walibya kama mateka mikononi mwa makundi yenye itikadi kali'', alisema rais huyo wa Misri.
Aidha, rais Abdel Fattah al-Sissi aliyataka makundi ya wanamgambo kusalimisha silaha zao, huku pia akitoa wito wa kuipa silaha serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa ambayo iliweka makao yake katika mji wa Mashariki wa Tobruk baada ya mji mkuu-Tripoli kutekwa na wapinzani wao.
Tayari serikali hiyo imekwishaomba kuondolewa kwa vikwazo vya kimataifa kuhusu silaha, ili iweze kudhibiti hali ya mambo katika nchi inayokabiliwa na machafuko.
Umoja wa Ulaya wajiweka kando
Hata hivyo jana Umoja wa Ulaya ulisema haufikirii mchango wowote katika uingiliaji kijeshi nchini Libya, na kuongeza kuwa ungefanya majadiliano na Marekani na Misri juu ya hatua za kuchukuliwa.
Kamishna wa umoja huo anayehusika na sera za kigeni Federica Mogherini alisema Ulaya inaitazama Libya kama nchi yenye vitisho vya aina mbili, kwanza kama taifa linalosambaratika, na pili kama nchi ambamo Dola la Kiislamu limejipenyeza na kuchukua hatamu.
Umoja wa Afrika kwa upande wake umeendelea kusisitiza kuwa mzozo wa Libya unaweza kusuluhishwa tu kupitia njia ya mazungumzo.
Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFPE
Mhariri:Yusuf Saumu