Al-Shabaab yaua wengine 10 Kenya
17 Juni 2014Tayari kundi hilo lenye mafungamano na al-Qaida limedai kuhusika na mashambulizi hayo, likisema wapiganaji wake walikivamia kijiji kimoja karibu na Mpeketoni na kwamba kikosi chake cha makamando kimefanikiwa kurudi kwenye kituo chao bila ya upinzani wowote baada ya siku mbili za operesheni zilizopelekea vifo vya Wakenya 60.
"Tulifanya mashambulizi mengine usiku wa jana. Tuliuwa watu 20, wengi wao polisi na askari wa wanyama pori. Makamando wamekwenda maeneo kadhaa wakiwasaka maafisa wa kijeshi," msemaji wa kijeshi wa al-Shabaab, Abdulaziz Abu Munsab, ameliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu.
"Makamando wametimiza wajibu wao na kurudi salama kwenye kituo chao," aliongeza, bila ya kusema ikiwa washambuliaji hao bado walikuwa ndani ya Kenya au walishavuuka mpaka na kuingia Somalia, umbali wa kilomita 100 kaskazini mwa Kenya.
Polisi ya Kenya yathibitisha
Polisi walithibitisha kwamba watu wenye silaha, wanaoonekana kuwa ni wale wale waliofanya mauaji ya takribani watu 50 kwenye mji wa Mpeketoni usiku wa kuamkia Jumapili, walikishambulia kijiji cha Poromoko, ambacho pia kimo kwenye Kaunti ya Lamu, usiku wa Jumatatu, lakini wamedai kuwa waliotibitika kuuawa hadi sasa ni watu 10.
Msemaji wa polisi, Zipporah Mboroki, alithibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo mapya, ambayo yamejiri huku maafisa wa ngazi za juu wa serikali wakielekea kwenye eneo hilo kuratibu operesheni za usalama. Afisa mmoja wa kaunti hiyo na polisi wa eneo hilo nao wanasema waliokufa ni watu 10.
Hata hivyo, Mboroki ameiambia AFP kwamba maafisa wao "wanajaribu kulifikia eneo la tukio na taarifa za undani bado hazijawa za kuaminika."
Mauaji ya Mpeketoni
Mashambulizi ya usiku wa Jumapili kwenye eneo hilo lililo karibu na eneo lenye hoteli nyingi za kitalii huko Lamu yalikuwa mabaya zaidi kufanyika ndani ya ardhi ya Kenya tangu kuzingirwa kwa jengo la maduka la Westgate jijini Nairobi mwezi Septemba, ambapo watu 67 waliuawa.
Mashahidi walisimulia namna wanamgambo wa al-Shabaab walivyoingia kwenye mji huo wenye Wakristo wengi na kukishambulia kituo cha polisi na kisha kuelekea kwenye hoteli na nyumba za watu. Washambuliaji hao pia waliwatenganisha Waislamu na wasio Waislamu, huku wakiwaacha bila ya kuwadhuru mateka wao walio Waislamu.
"Walikuja na kuwataka watu watoke nje. Waliwaamuru kulala chini na kuwapiga risasi kichwani mmoja baada ya mwengine," alisema David Waweru, ambaye alikuwa akiangalia mechi ya Kombe la Dunia katika mkahawa mmoja lakini akafanikiwa kujificha nyuma ya nyumba wakati mashambulizi ya Mpeketoni yalipoanza.
"Kisasi kwa ukatili wa serikali ya Kenya"
Al-Shabaab mashambulizi hayo ni kulipiza kisasi uwepo wa wanajeshi wa Kenya nchini Somalia na pia "unyama wa serikali ya Kenya dhidi ya Waislamu nchini humo kupitia vitisho, mateso na mauaji ya maulamaa wa Kiislamu."
Wanajeshi wa Kenya walivuuka mpaka na kuingia kusini mwa Somalia mwaka 2011 kupambana na al-Shabaab, na baadaye kujiunga na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini humo (AMISOM), kilichopelekwa huko kupambana na wanamgambo hao na kuisaidia serikali mjini Mogadishu inayoungwa mkono kimataifa.
Maulamaa kadhaa wanaoaminika kuwa na misimamo mikali wameuawa kwenye mji wa bandari wa Mombasa katika miaka ya hivi karibuni, huku makundi ya haki za binaadamu yakiishutumu serikali ya Kenya kwa kufanya mauaji ya makusudi.
Al-Shabaab pia waliitangaza Kenya kuwa ni "medani ya kivita" na kuwaonya watalii na wageni kuondoka kwenye nchi hiyo, ambao iliwaji kuwa kituo kikuu cha utalii lakini sasa ikikabiliwa na anguko kubwa kwenye mapato yatokanayo na biashara hiyo kutokana na mizozo ya kisiasa, kuongezeka kwa uhalifu na wimbi la mauaji na mashambulizi yanayotuhumiwa kufanywa na al-Shabaab.
"Wageni wanaojali usalama wao wanapaswa kuondoka Kenya au vyenginevyo wakabiliane na machungu ya ukaidi wao," ilisema al-Shabaab kwenye taarifa yake ya Jumatatu.
"Hivyo tunaionya serikali ya Kenya na raia wake kwamba madhali munaendelea kuivamia nchi yetu na kuwakandamiza Waislamu wasio hatia, mashambulizi yataendelea na uwezekano wa amani na utulivu nchini Kenya utakuwa ndoto," lilisema kundi hilo.
Waandishi wa habari walio mjini Mpeketoni wanasema hali kwenye mji wa Mpeketoni ilikuwa ya wasiwasi sana hadi Jumanne, huku wakaazi wa huko wakihofia mashambulizi mapya licha ya kuwapo kwa polisi na wanajeshi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman