1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Shabaab washambulia bunge Somalia

25 Mei 2014

Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa limeeleza kuchukizwa kwake,baada ya waasi wa al-Shebaab kufanya shambulio dhidi ya bunge la Somalia ambapo watu kiasi 10 wameuwawa siku ya jumamosi(24.05.2014).

https://p.dw.com/p/1C6OO
Bildergalerie Somalia Sicherheitslage Shebab Anschlag 2013
Shambulio lililofanywa na al-Shabaab mjini MogadishuPicha: Mohamed Abdiwahab/AFP/Getty Images

Duru za kiusalama nchini humo zimesema kuwa shambulio hilo lililohusisha mashambulizi ya mabomu na watu wenye silaha wakiwa wamevaa miripuko hatimaye lilifikishwa mwisho baada ya zaidi ya saa nne za mapambano na majeshi ya Somalia na jeshi la mataifa ya Afrika la kulinda amani.

Wajumbe 15 wa baraza la usalama wamesema "wachukizwa kwamba kundi la al-Shabaab limeshambulia bunge la shirikisho, taasisi ambayo inawakilisha watu wa Somalia na matumaini yao halali ya amani, usitawi na uthabiti."

Somalia Anschlag in Mogadischu 24. Mai 2014
Wanjajeshi wakimuokoa mtu aliyejeruhiwa baada ya shambulioPicha: Reuters

Shambulio hilo ambalo lilisababisha umwagikaji wa damu , pamoja na matukio mengine ya kiwenda wazimu ya kigaidi , hayatapunguza , "uungaji mkono wao kwa jeshi la kulinda amani la mataifa ya Afrika AMISOM pamoja na wahusika wengine wanaopigania amani nchini Somalia, wamesema.

Katibu mkuu ashutumu shambulio

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon pia ameshutumu shambulio hilo, akielezea "mshikamano na uungaji mkono wake " kwa wabunge.

"Hakuna uhalali wowote kwa shambulio kama hilo," amesema.

Somalia Anschlag in Mogadischu 24. Mai 2014
wanajeshi wakiendelea kupambana na al-ShabaabPicha: Reuters

Hakuna idadi kamili ya watu waliouwawa iliyotolewa mara moja lakini maafisa wa polisi na duru za serikali zimesema kuwa watu 10 , ikiwa ni pamoja na washambuliaji kadha , wamethibitishwa kuwa wameuwawa.

Vyombo vya habari vya ndani vimesema watu zaidi ya 20 huenda wameuwawa, ikiwa ni pamoja na washambuliaji wanane. Msemaji wa kundi la al-Shabaab amethibitisha kuwa kundi hilo linahusika na shambulio hilo.

Waziri ajiuzulu

Wakati huo huo waziri wa Somalia anayehusika na usalama Abdikarim Hussein Gulled ametangaza kujiuzulu jana Jumamosi(24.05.2014) baada ya shambulizi hilo la kundi lenye msimamo mkali wa Kiislamu na kusababisha zaidi ya watu 24 kuuwawa katika shambulio lililotokea katika jengo la bunge.

Gulled ametoa tangazo hilo katika redio ya taifa mjini Mogadishu, Hakusema sababu ya kujizulu kwake, lakini amekuwa katika mbinyo kutoka kwa bunge kuhusiana na hali inayoendelea ya kutokuwa na usalama katika taifa hilo. Wakosoaji wamesema kwamba Gulled anakosa uzoefu katika nyanja hiyo ya usalama.

Rais arejea nyumbani

Rais Hassan Sheikh Mohamud amefupisha ziara yake nchini Afrika kusini, ambako alihudhuria kuapishwa kwa rais Jacob Zuma kwa kipindi cha pili cha utawala, akisema atarejea nyumbani leo Jumapili (25.05.2014).

Zaidi ya watu 30 wamejeruhiwa, ikiwa ni pamoja na wanajeshi 14 wa jeshi la Somalia pamoja na wanajeshi watano wa jeshi la Afrika la kulinda amani.

Serikali ya Somalia imekuwa ikipambana na kundi la al-Shabaab kwa miaka kadha sasa kwa msaada wa jeshi la mataifa ya Umoja wa Afrika.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe

Mhariri: Abdu Mtullya