Al-Shabaab wakaribia kuipoteza Kismayo
28 Septemba 2012"Lengo la AMISOM ni kuwakomboa watu wa Kismayo na kuwawezesha kuendelea na maisha yao kwa amani, utulivu na usalama. Operesheni zetu zinaendelea kulenga shabaha maalum za al-Shabaab mjini Kismayo," alisema Kamanda Andrew Gutti wa AMISOM, akiwataka wapiganaji wote wa al-Shabaab walio ndani ya Kismayo kuweka chini silaha zao.
Katika hatua nyengine, Jeshi la Kenya limesema kwamba wapiganaji wake wamelichukua eneo la kusini ya Kismayo, ngome ya mwisho ya kundi la al-Shabaab.
Msemaji wa Jeshi hilo, Cyrus Oguna, aliliambia shirika la habari mapema leo kwamba wanajeshi wa Kenya walikumbana na upinzani mdogo wakati wa kuliteka eneo hilo.
Al-Shabaab, wakaazi wa Kismayo wakanusha
Hata hivyo, wakaazi wa huko pamoja na wanamgambo wa al-Shabaab wamekanusha taarifa hizo, wakisema kwamba ndio kwanza wanajeshi wa Kenya walikuwa kwenye viunga vya mbali na Kismayo, ambako wamekuwako kwa zaidi ya siku nne sasa.
"Maadui wakitumia mashua za kijeshi walituma mamia ya wanajeshi katika eneo la pwani jana usiku na mujahidina wetu wanakabiliana nao katika mapigano makali hivi sasa," alisema kamanda wa al-Shabaab, Sheikh Mohamed Abu Fatuma, akisisitiza kuwa umbali walipo wanajeshi wa Kenya ni kiasi ya maili sita kutoka Kismayo.
Wakaadhi kadhaa pia wa Kismayo walisema kwamba wanajeshi wa Kenya bado walikuwa ufukweni, walikotia nanga wakiwa kwenye mashua mbili zilizosindikizwa na helikota za kijeshi, umbali wa kilomita tano kutoka katikati ya mji.
"Mji wenyewe bado uko chini ya udhibiti wa al-Shabaab. Radio Andalus inaendelea kufanya kazi, ikiwataka watu kujitokeza kujiunga na jihadi na kuwafukuza wavamizi," alisema mmoja wa wakaazi hao, Abdulahi Yakub.
Kismayo ni ngome kuu ya mwisho ya al-Shabaab
Mji wa bandari wa Kismayo ni ngome kuu ya mwisho mikononi mwa al-Shabaab, ambao tayari wameshapoteza ngome zao nyengine - ikiwemo miji ya Afgoye, Baidoa na Marka - kwa kikosi cha wanajeshi 17,000 wa Umoja wa Afrika, kinachojumuisha pia wanajeshi wa Kenya na Ethiopia.
Jumanne iliyopita (tarehe 25 Septemba) jeshi la Kenya liliushambulia uwanja wa ndege wa Kismayo kwa ndege za kijeshi, ikiwa ni sehemu ya operesheni kuu ya kuingia mji huo.
Tangu wanajeshi wa Kenya walipoingia nchini Somalia mwaka jana kupambana na al-Shabaab, wamekuwa wakilenga kuuchukua mji huo. Lakini kufikia lengo hilo kumewachukua muda mrefu zaidi kuliko walivyokuwa wametarajia.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/DPA
Mhariri: Othman Miraji