Matokeo ya uchaguzi kutangazwa leo
26 Machi 2010Waziri mkuu wa Iraq Nuri al-Maliki, muasi wa zamani aliyeishi uhamishoni kwa muda mrefu sasa anaonekana kuwa mdhaifu kisiasa saa chache tu kabla ya matokeo ya uchaguzi wa tarehe saba mwezi huu kutangazwa.
Al-Maliki amesisitiza kwamba hesabu ya kura ifanyike tena baada ya chama cha mpinzani wake cha Iraqiya kuonekana kupata kura nyingi kuanzia mwanzo wa shughuli ya kuhesabu kura. Tume ya uchaguzi nchini humo ilipuuzilia mbali azimio lake licha ya Maliki kusema kwamba huenda uamuzi wa tume unaweza ukairejesha Iraq katika ghasia.
Maliki ni mwanasiasa mwenye asili ya Kishia, mzaliwa wa mkoa wa Hilla mwaka wa 1950.
Naye mpinzani wake, waziri mkuu wa zamani Iyad Allawi alianza kurejea katika uwanja wa kisiasa baada ya nchi hiyo kutoka katika vita. Ni tabibu wa miaka 64. Mwanzoni mwa uchaguzi wa mapema mwezi huu, Allawi alilalamika kwamba utaratibu uliotumiwa na tume hiyo haukufaa na aliikashifu tume ya uchaguzi kwa kuzembea licha ya msururu wa malalamiko kutoka kwa viongozi wa vyama vya kisiasa kuhusu wizi wa kura na kukiukwa kwa sheria zingine za uchaguzi.
Viongozi hao wawili ndio wanaomurikwa zaidi muda mfupi kabla ya matokeo ya kura kutangazwa hii leo. Waziri mkuu wa sasa Nuri al-Maliki anayeungwa mkono na wafuasi wengi wa kutoka katika madhehebu ya Washia anakumbwa na upinzani mkali kutoka kwa Iyad Allawi anayesifika sana katika kabila la wachache la Wasunni.
Ikiwa hakutakuwa na ushindi dhahiri katika matokeo hayo, wachunguzi wa kisiasa wanadai kwamba huenda demokrasia katika serikali itakuwa dhaifu na kukawa na shinikizo za muungano wa vyama na hatimaye kuchangia katika kuleta machafuko.
Waziri wa ndani wa Iraq, Jawad al-Bolani alisema jana kwamba tume ya uchaguzi inafaa kuchelewesha matangazo ya matokeo ya kura leo ili kuwapa nafasi mahasimu wa kisiasa muda wa kujadiliana na kuafikiana. Tume ya uchaguzi inafaa kutangaza matokeo ya uchaguzi siku kumi na tisa baada ya tarehe saba, upigaji kura ulipokamilika.
Mkuu wa tume ya uchaguzi nchini Iraq, Faraj al-Haidari amesema kwamba ushindi kati ya wapinzani wakuu al-Maliki na Allawi utakuwa pengine wa kiti au viti viwili, ishara madhubuti kwamba upinzani ni mkali na kutazuka ubishi mkali.
Matokeo ya muda siku ya Jumapili ilionyesha Allawi akiwa na kura 11,000 mbele ya al-Maliki, waziri mkuu wa sasa baada ya asilimia 95 ya kura milioni 12 iliyopigwa kuhesabiwa. Wachunguzi wa kisiasa wanasema wanatarajia vyama vikuu viwili kushinda asilimia 90 ya viti katika bunge ambalo lina viti 325.
Kwa siku za hivi karibuni vyama vikuu vya kisiasa vimekuwa vikifanya mikutano ya faragha kabla ya matokeo kutangazwa katika kile kinachohusishwa na mikakati ya kuunda serikali ya muungano.
Wakati huo huo, wanamgambo nchini Iraq wameanza kujitokeza na kujaribu kusambaratisha shughuli za kisiasa kwa kuripua mabomu. Polisi waliwaua wanamgambo wawili katika eneo la Qada al-Hadar, kusini mwa mji wa Mosul ulioko kaskazini mwa nchi hiyo.
Mwandishi, Peter Moss /Reuters/AFP/AP/DPA
Mhariri:Aboubakary Liongo