1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Bashir ahukumiwa kifungo cha miaka miwili

14 Desemba 2019

Mahakama nchini Sudan imemkuta Rais wa zamani Omar al-Bashir na hatia ya makosa ya utakatishaji fedha na rushwa na kumhukumu kifungo cha miaka miwili katika kizuizi chenye ulinzi mdogo

https://p.dw.com/p/3UnoZ
Sudan Khartum | Prozess & Urteil Omar al-Baschir, ehemaliger Präsident
Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/M. Hajaj

Hiyo ni hukumu ya kwanza katika msururu wa kesi zinazomkabili al-Bashir, ambaye pia anasakwa na mahakama ya Kimataifa ya Jinai – ICC kuhusiana na mashitaka ya uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki yanayohusiana na mgogoro wa Darfur katika miaka ya 2000.

Hukumu ya leo inakuja ikiwa ni mwaka mmoja baada ya waaandamanaji nchini Sudan kuanzisha vuguvugu la mapinduzi dhidi ya serikali ya kimabavu ya al-Bashir. Wakati wa miongo yake mitatu madarakani, Sudan iliwekwa kwenye orodha ya Marekani kwa kufadhili ugaidi, na uchumi wa nchi hiyo ukasambaratishwa na miaka mingi ya usimamizi mbaya na vikwazo vya Marekani.

Sudan Khartum | Prozess & Urteil Omar al-Baschir, ehemaliger Präsident
Hali ilivyokuwa mahakamani wakati wa kusomwa hukumuPicha: picture-alliance/Anadolu Agency/M. Hajaj

Al-Bashir amekuwa kizuizini tangu Aprili, wakati jeshi la Sudan lilimuondoa madarakani baada ya miezi kadhaa ya maandamano ya kitaifa. Mapinduzi hayo kisha yakalizimisha jeshi kugawana madaraka na raia.

Jkeshi la Sudan limesema halitompeleka katika mahakama ya ICC. Serikali ya mpito inayojumuisha jeshi na raia haijadokeza kama watamkabidhi katika mahakama ya The Hague.

Chama cha Wasomi cha Sudan ambacho kiliongoza vuguvugu la maandamano, limeupongeza uamuzi wa leo wa mahakama kikisema ni "hukumu ya kiimadili na kisiasa”, dhidi ya rais huyo wa zamani na utawala wake.

Chini ya sheria ya Sudan, al-Bashir mwenye umri wa miaka 75, atapelekwa katika kituo kinachosimamiwa na serikali cha wazee wanaohukumiwa kwa uhalifu ambao adhabu yake sio ya kifo. Lakini atasalia gerezani wakati kesi yake ya mashitaka mengine ikiendelea kuhusiana na mauaji ya waandamanaji katika miezi iliyotangulia kuangushwa kwake.

Sudan Khartum | Prozess & Urteil Omar al-Baschir, ehemaliger Präsident | Anhänger
Wafuasi wa al-Bashir wakiandamana mjini KhartoumPicha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Mamia ya wafuasi wa al-Bashir pia waliandamana karibu na kasri la rais mjini Khartoum, ambako vikosi vya usalama vilizuia barabara za kuingia katika kasri hilo na makao makuu ya jeshi.

Wakili wake Mohammed al-Hassan alisema hukumu hiyo ya leo ilitarajiwa na kuwa kesi ya rufaa itawasilishwa katika mahakama ya juu, akiongeza kuwa "motisha wa rais huyo wa zamani upo juu.”

Baada ya kuondoshwa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi ya Aprili 11, al-Bashir aliweza kubainika kuwa na kiwango kikubwa cha fedha nyingi za ndani na za kigeni sambamba na mali nyingine pasipo na hati za kisheria za umiliki. Pamoja na kwamba alikiri kupokea dola milioni 25 kutoka kwa Mwanamfalme Bin Salman wa Saudi Arabia, lakini hajayakubali makosa kwa mashitaka yanayomkabili.