1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al Ahly ndio mabingwa wapya wa vilabu Afrika

Admin.WagnerD12 Novemba 2013

Al Alhy ya Misri imepata taji lake la nane la mataifa ya Afrika la Champions League ilipoizamisha Orlando Pirates ya Afrika Kusini mabao 2-0 katika mchezo wa duru ya pili mjini Cairo

https://p.dw.com/p/1AFvI
Picha: picture-alliance/dpa

Al Ahly ambayo hapo kabla ilishinda kombe la mabingwa wa Afrika mwaka 1982, 87 , 2001, 2005, 2006, 2008 , 2012, ilipata ushindi wa jumla ya mabao 3-1 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza mjini Johannesburg.

Mashetani wekundu hao wa mjini Cairo wamepata kitita cha euro milioni 1.5 na pia italiwakilisha bara la Afrika katika michuano ya FIFA ya ubingwa wa dunia kwa vilabu nchini Morocco mwezi ujao.

Mchezaji wa kiungo wa Manchester City Yaya Toure ana nafasi nyingine ya kupata tuzo ya mchezaji bora wa bara la Afrika inayodhaminiwa na shirika la utangazaji wa BBC baada ya kufanikiwa kuwa katika orodha ndogo ya wachezaji wanaoweza kupata tuzo hizo.

Katibu mkuu wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Jerome Valcke anakutana na waziri wa michezo wa Ghana pamoja nma maafisa wengine nchini Togo leo kuwahakikishia mipango wa usalama kwa ajili ya mchezo wa mtoano katika kinyang'anyiro cha kuwania tikiti ya kucheza katika fainali za kombe la dunia mwakani nchini Brazil mchezo ambao utafanyika mjini Cairo wiki ijayo.

Ghana ilisema kuwa inahofia usalama nchini Misri baada ya mara kwa mara nchi hiyo kukumbwa na maandamano na huenda mashabiki wa Misri wakafanya maandamano dhidi ya utawala wa kijeshi nchini humo katika uwanja wa mjini Cairo wa Juni 30 ambao unamilikiwa na jeshi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre / ape /afpe

Mhariri: Mohammed Khelef