1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al Abadi kufanya mazungumzo na Obama nchini Marekani

Admin.WagnerD14 Aprili 2015

Waziri mkuu wa Iraq Haidar al Abadi na Rais wa Marekani Barack Obama leo watajadili kuhusu namna za kupambana dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la dola la kiislamu IS katika Ikulu ya Rais wa marekani.

https://p.dw.com/p/1F837
Picha: AFP/Getty Images

Katika ziara yake ya kwanza tangu kuwa Waziri mkuu wa Iraq, al Abadi anatarajiwa kuomba msaada wa mabilioni ya fedha wa ndege za kijeshi zisiondeshwa na marubani na silaha nyingine kutoka kwa Marekani ili kupambana na wanamgambo wa IS ambao wanayadhibiti maeneo mengi kaskazini na kati mwa Iraq tangu mwaka jana.

Utawala wa Obama ambao ulipokea vyema kuingia madarakani kwa al Abadi baada ya kuwa na uhusiano tete na mtangulizi wake Nuri al Maliki, huenda usiridhie maombi yote ya misaada ya kijeshi kutoka kwa Iraq.

Marekani yamkubali al Abadi

Hata hivyo mkutano huo muhimu kati ya viongozi hao wawili katika ofisi ya Rais Obama unamaanisha kuwa Marekani imemkubali al Abadi kama kiongozi wa Iraq kwani anajaribu kushirikisha maoni ya kutoka nje kumliko al Maliki kuhusu jinsi ya kuiendesha Iraq.

Rais wa Marekani Barack Obama
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: AP

Obama mnamo mwezi Agosti mwaka jana, aliidhinisha kuanzishwa mashambulizi ya angani nchini Iraq tangu majeshi ya nchi yake kuondoka nchini humo mwaka 2011 na amewatuma wanajeshi 3,000 nchini humo kutoa mafunzo na ushauri kwa majeshi ya Iraq na wapiganaji wa kikurdi wanaopambana na wanamgambo wa IS.

Msemaji wa ikulu ya Rais wa Marekani Josh Ernest amesema iwapo kuna mawazo makhususi kutoka kwa waziri mkuu wa Iraq ya kuongezewa misaada, basi Marekani itayazingatia kwa makini.

Ernest amesema lengo bila shaka ni kuendeleza ushirikiano mkubwa ambao tayari upo kati ya Marekani na Iraq na ni ushirikiano ambao Marekani umewekeza pakubwa.

Ushawishi wa Iran pia kujadiliwa

Obama na al Abadi pia wanatarajiwa kuzungumzia wajibu wa Iran katika vita hivyo dhidi ya wanamgambo wa kundi la dola la kiislamu IS. Makundi ya wanamgambo wa kishia wanaoungwa mkono na Iran yamekuwa na mchango mkubwa katika kupambana na IS nchini Iraq na katika nchi jirani ya Syria.

Wanajeshi wa Marekani nchini Iraq
Wanajeshi wa Marekani nchini IraqPicha: Getty Images/J. Moore

Serikali ya Marekani imeelezea wasiwasi kuhusu makundi hayo ya wanamgambo wa kishia ambao wanashutumiwa kwa kufanya uovu dhidi ya jamii ya wasunni wakiarabu walio wachache ambao wanawaunga mkono wanamgambo wa IS.

Maafisa wa serikali ya Iraq wamesema wanapanga operesheni kubwa dhidi ya IS katika ngome zao mbili kuu katika jimbo la Anbar lililoko magharibi mwa Iraq na katika mji wa Mosul ulioko kaskazini mwa nchi hiyo.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman