1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ajali ya Tupolov yaagharimu maisha ya viongozi kadhaa wa Poland

Oumilkher Hamidou12 Aprili 2010

Poland iko msibani baada ya rais wao na mkewe,naibu spika wa bunge,viongozi wa jeshi ,mkuu wa benki kuu na wabunge kadhaa kuuwawa katika ajali ya ndege

https://p.dw.com/p/Mthj
Wapoland wanaweka mishumaa na mauwa mbele ya kasri la rais kuwakumbuka wahanga wa ajali ya ndegePicha: AP

Mada moja tuu imepewa umbele na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo: Msiba mkubwa ulioisibu Poland baada ya rais Lech Kaczynski,mkewe,wabunge kadhaa na viongozi kadhaa wa kiuchumi na kijeshi kuanguka,watu 97 kuiaga dunia kufuatia ajali ya ndege !Licha ya msiba huo mkubwa, msaada wa Umoja wa ulaya kwa Ugiriki ni miongoni mwa yaliyochambuliwa magazetini.

Tuanzie basi na gazeti la !Allegemeine Zeitung" la mjini Mainz linalojiuliza eti kweli historia ya dunia inaweza kuwa ya kibeuzi?

"Hadi sasa jibu ni ndio!Rais wa Poland amefariki dunia alipokua njiani kwenda kule ambako miaka 70 iliyopita,maelefu ya wapoland waliuliwa na watumishi wa idara ya upelelezi ya Urusi-katika mji wa Katyn.Poland inalazimika kwa mara nyengine tena kumeza machungu ya majaaliwa-kama ilivyotokea mara kadhaa katika historia yake.Matumaini yaliyopo ni kwamba wapoland kila wakati wanapiga moyo konde na kusimama wima kupigania mustakbal wao.Katika vita vikuu vya pili vya dunia hali ilikua hivyo hivyo pale Hitler alipoivamia nchi hiyo na kusababisha mauwaji ya kikatili kabisa chanzo cha kuuliwa mayahudi milioni sita. Mwaka 1980 pia pale chama cha kwanza huru cha wafanyakazi,katika kambi ya mashariki,Solidarnosc-kilipolazimika kusabilia wafuasi wake kadhaa,ili kujenga msingi wa demokrasia,miaka kadhaa kabla ya ukuta wa Berlin kuporomoka.Matumaini yamechomoza pia safari hii kwasababu Urusi inaomboleza pia pamoja na jirani yake."

Gazeti la "Lausitzer Rundschau" la mjini Cottbus linaandika

"Mandhari yote ya kisiasa na kijamii itabadilika nchini Poland kwasababu walioangukia mhanga wa ndege hiyo chapa ya Tupolew,sio tuu wabunge kadhaa wa chama cha PiS,bali pia viongozi kadhaa wa mrengo wa kulia nchini Poland.Miongoni mwa wanachama wa chama cha PiS ni pamoja na mwenyekiti wa benki kuu ya Poland Slawomir Skrzypek ambae sawa na ndugu mapacha-Kaczynski hakua akipendezewa na sarafu ya ulaya-Yuro.Serikali ya waziri mkuu Tusk ilitaka sarafu hiyo ianze kutumika haraka.Kwa hivyo kiongozi mpya wa benki kuu ya Poland anaweza kuleta mageuzi.

Gazeti la "Der neue Tag" la mjini Weiden linahimiza mshikamano na kuandika:

"Muhimu kwa nchi zilizosalia za Ulaya na hasa Ujerumani,katika wakati huu mgumu ni kwa majirani wote na wanachama wote wa umoja wa Ulaya kuionyesha Poland haiko peke yake.

Magazeti ya Ujerumani yamezungumzia pia uamuzi wa mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya wa kuisaidia Ugiriki.Gazeti la "Nürnberger Zeitung" linaandika

Ugiriki ikitetereka tuu,basi mataifa mengine ya Umoja wa Ulayayanayodaiwa kupita kiasi,mfano Ureno na Hispania yataporomoka mfano wa nyumba ya karata na kwa namna hiyo kuitia hatarini sarafu Yuro-licha ya kwamba hivi sasa ni imara.Ndio maana nchi za zoni ya yuro zinabidi kuwajibika na kuimarisha mpango wa kuisaidia Ugiriki.Pupa wala hadaa,hazitasaidia kitu.Na huo hasa ndio mwito uliotolewa jana na mawaziri wa fedha wa zoni ya yuro.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Imepitiwa na: Saumu Mwasimba