1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ajali ya ndege Brazil yaua kiasi watu 200

18 Julai 2007

Inahofiwa watu hadi 200 wamefariki dunia katika ajali ya ndege iliozuka Sao paulo hapo jana.

https://p.dw.com/p/CB2k
Jamaa wa abiria wataka habari kwenye uwanja wa ndege wa Sao Paolo
Jamaa wa abiria wataka habari kwenye uwanja wa ndege wa Sao PaoloPicha: AP

Airbus chapa A320 iliteleza ikitua kwenye uwanja uliokua na maji ikagonga vizuwizi vya uwanja wa ndege na kuingia katika barabara kuu ya magari kabla kusimama mbele ya kituo cha kuuzia mafuta ya petroli na kuzuka mripuko.

Abiria wote 176 wanahofiwa wamefariki na si chini ya watu wengine 15 wameuwawa ardhini .

Ikiwa idadi hiyo ya wa´naodhaniwa kufariki itathibitika baadae,hii itakua ajali mbaya kabisa ya ndege katika historia ya Brazil.

Watumishi wa shughuli za uokozi na madaktari na maafisa wa usalama wakihifadhi mabaki ya ndege hiyo.

Ndege hii ilikua njiani ikielekea mjini Sao Paulo kutoka Porto Alegre,kusini mwa Brazil ilipojigonga na kuripuka moto ikitua huku mvua ikinyesha.

Ajali hii ilizuka muda mfupi kabla ya saa moja za jioni –saa za Brazil.Ndege hii ilijigonga moja kwa moja na jumba kwenye uwanja huo wa ndege huku ikiwaka moto.Ni sehemu tu ya ndege hiyo inayoweza sasa kuonekana.

Wazimamoto hivi sasa wamefaulu kuzima moto na magari ya kuchukua wagonjwa hospitali yakitibu waliojeruhiwa.Hivi sasa uwanja wa ndege huo wa Congonhas um,efungwa kikamilifu na safari zote za ndege zimefutwa kutokana na msiba huo au zimehamishiwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sao Paulo.

Bado si wazi nini hasa chanzo cha ajali hii.Hatahivyo, juzi tu jumatatu, ndege ya shirika la ndege la Brazil-Pantanal- iliteleza wakati ikitua na baadae ikajikuta imekwama.

Uwanja huu wa ndege ulifunguliwa tena kutumika siku chache tu nyuma baada ya matengenezo ya kuutia lami mpya.Ni wakuu wa uwanja wa ndege waliotoa ruhusa ya kutumika tena.Kwa muujibu wa shahidi mmoja,kulikuwapo kidimbwi kidogo cha maji katika njia ya kutua ndege.

Tangu kujigonga ndege ya shirika la ndege la Brazil la GOL na ile ya Marekani-FIRMENJET hapo Septemba 2006 ambamo watu 154 walifariki dunia, huu ndio msiba mkubwa kabisa kuwahi kuzikumba safari za ndege nchini Brazil.

Rais Lula da silva wa Brazil,alieitisha kikao cha dharura cha baraza lake la mawaziri,ametangaza tanzia la siku 3 kuomboleza waliofikwa na ajali hii.Sasa maswali mengi yataulizwa juu ya hali ya uwanja huu wa ndege na kwanini ukaruhusiwa kutumika tena.