Ahadi ya Obama kwa viongozi wa nchi za Ghuba
15 Mei 2015Katika mkutano wa kilelle uliyofanyika Alhamisi nchini Marekani pamoja na Rais Obama, nchi za Ghuba zimeeleza hofu yao juu ya makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na Marekani ambayo yatapunguza uwezo wa kinyuklia wa Iran na kuondolewa kwa vikwazo vya kimataifa. Nchi hizo zinaamini makubaliano ya mpango wa nyuklia yatafufua uchumi wa taifa hilo na kuliwezesha kutengeneza silaha imara zaidi za makombora.
Taarifa ya pamoja ya nchi za Ghuba kufuatia mkutano huo wa kilele imesema, nchi hizo kwa pamoja zina dhamira ya kuunda mfumo wa ulinzi wenye uwezo wa kupambana na makombora ikiwamo pia mfumo wa tahadhari wa mapema ambao utahitaji msaada wa kiufundi kutoka Marekani. Mfumo wa ulinzi wa rada wapamoja kati ya nchi za ghuba, utaziwezesha nchi hizo kupambana na Iran iwapo itajaribu kufanya mashambulizi ya makombora dhidi yao.
Marekani imeahidi kupeleka silaha kwa nchi hizo pamoja na kutuma timu ambayo itafanya mazungumzo ya kina na nchi hizo katika wiki zijazo.
Kwa upande wake Obama amezihakikishia nchi za kiarabu kuwa wako salama kutokana na kitisho cha kushambuliwa na Iran. Lakini bado Obama hakuweza kupata uhakika wa ushirikiano wa nchi za kiarabu, katika mkataba wa nyuklia na Iran unaotegemewa kuafikiwa mwezi Juni.
Obama ameahidi kuzilinda nchi za kiarabu pamoja na kupeleka vikosi vya kijeshi iwapo nchi hizo zitavamiwa na Iran ama taifa lengine lolote.
"Sote tuna wajibu. Na hapa leo katika eneo la Camp David, tuliamua kupanua ushirikiano wetu kwa njia mbalimbali muhimu. Kwanza, ninahakikisha dhamira ya Marekani ya kuhakikisha usalama wa washirika wetu wa nchi za Ghuba. Kama tulivyotangaza katika taarifa ya pamoja, Marekani iko tayari kufanya kazi kwa pamoja na mataifa ya nchi za ghuba kuzuia na kukabiliana na tishio la nje kwa taifa lolote ambalo haliendani na mkataba wa Umoja wa Mataifa," amesema Obama.
Hata hivyo kwa upande wa nchi za Ghuba wanailaumu Iran kwa mzozo unaoendelea nchini Yemen na kusema kuwa mkataba wa nyuklia utaipa Iran nguvu zaidi za kiuchumi.
Nchi hizo za kiarabu zinaishutumu Iran kuwasaidia wanamgambo wa kihuthi ambao wameshikilia maeneo kadhaa nchini Yemen na wana wasiwasi kuinuka kiuchumi kwa Iran kutapelekea vurugu kuendelea zaidi Yemen.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/ RTRT/APE
Mhariri:Josephat Charo