Afrika yatoa sauti katika mkutano wa COP23
9 Novemba 2017Mataifa ya Kiafrika pamoja na mashirika yanafanya juu chini kuhakikisha kuwa uwepo wao katika mkutano huu wa kilele ni mkubwa kwa kuelezea wasiwasi wao na mawazo yao na sasa yanatumia ushawishi wao ili kuyawekea shinikizo mataifa yaliyostawi kujitolea katika mipango ya kupunguza kiwango cha gesi ya mkaa, kwa ajili ya maeneo maskini na yaliyo katika hatari kubwa.
Afrika ni bara ambalo huenda likaathirika kwa kiasi kikubwa na mabadiliko za tabianchi, huku karibu thuluthi mbili ya idadi ya watu wake wakijipa kipato kutokana na shughuli za kilimo.
Yunis Arikan, Kiongozi wa kundi linalojiita Advocacy and Development kutoka ICLEI – Local Governments for Sustainability) anaamini kuwa mataifa ya Afrika ya Kiafrika yamepaza sauti sana na kuchangamka katika mikutano ya Umoja wa Mataifa kuhus mabadiliko ya tabianchi tangu mkutano wa kwanza kabisa ulioandaliwa mjini Berlin mwaka wa 1995. Miongoni mwa Zaidi ya viongozi wetu 300, tuna ujumbe mkubwa kutoka Afrika unaoleta suluhisho na masuala ya kipaumbele.
"Nadhani, mkutano wa COP hapa Ujerumani unatimiza lengo lake la kuipa sauti Afrika na tuna furaha kubwa kwamba tunakuja hapa sio tu kusikiliza, bali kuzungumza na kutoa suluhisho zao na matarajio yao ili yawe sehemu ya mchakato na sio tu kama mtazamani”. Amesema Arikan.
Mataifa yaliyostawi yawajibishwe
Uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump kuiondoa Marekani katika Makubaliano ya Paris mapema mwaka huu umetawala majadiliano yanayojitokeza katika mkutano huu wa COP23 – hasa baada ya Syria kutangaza mipango yake ya kujiunga katika muafaka huo, na hivyo kuifanya Marekani kuwa nchi pekee inayopinga mkataba huo.
Lakini kwa mataifa mengi ya Afrika, kujiondoa kwa Marekani kunaonyesha kupuuzwa kabisa kwa mataifa maskini Zaidi ya Afrika ambayo huenda yakaathirika Zaidi kutokana na athari mbaya kabisa za mabadiliko ya tabianchi – hoja ambayo inaumiza sana kutokana na ukweli kwamba kiwango kikubwa cha gesi ya ukaa huzalishwa na mataifa tajiri, yaliyostawi kiviwanda, kama vile Marekani.
Muungano wa Nchi za Kiafrika zinazopigania haki katika masuala ya hali ya hewa – Panafrican Climate Justice Alliance – PCJA unayawakilisha mashirika ya kiraia barani humo. Rebecca Muna, kutoka shirika la Forum for Climate Change in Tanzania, ambalo ni sehemu ya muungano wa PCJA ameambia DW kuwa sehemu ya lengo la shirika hilo katika mkutano huu ni kuyashinikiza mataifa yaliyostawi kiviwanda kuweka malengo makubwa ya kupunguza gesi za ukaa ili mataifa ya Kiafrika yasikabiliwe na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi
Kundi hilo kupitia katibu wake mkuu Mithika Mwenda, anahoji uwepo wa ujumbe wa wawakilishi wa Marekani katika mkutano huo. Anahofia kuwa huenda ukawa na ushawishi mbaya kwa mataifa mengine ambayo bado hayajachukua hatua kubwa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kitu anachokiita "Athari ya Trump”.
Mwandishi: Ineke Mules/Bruce Amani/DW
Mhariri: Mohammed Khelef