Afrika yataka uchunguzi dhidi ya ukatili wa polisi Marekani
16 Juni 2020Nchi za Afrika zinapigia debe kuanzishwa uchunguzi kuhusu ubaguzi wa kimfumo na ukatili wa polisi nchini Marekani na kwingineko, zikilenga kutetea haki za watu wenye asili ya Afrika.
Waraka uliozungushwa miongoni mwa wanadiplomasia mjini Geneva unaelezea kushtushwa kwa nchi za kiafrika, na visa vya ukatili wa polisi dhidi ya watu waliokuwa wakiandamana kwa amani, kupinga kifo cha mmarekani mweusi, George Floyd aliyekufa akiwa mikononi mwa Polisi mjini Minneapolis. Kifo chake kilifuatiwa na maandamano makubwa katika sehemu nyingi za dunia, kupinga ukatili huo.
Soma zaidi: Mataifa ya Afrika yaomba mjadala kuhusu ubaguzi
Mwakilishi wa Burkina Faso katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjni Geneva Desire Sougouri, alisema tatizo hili la ubaguzi dhidi ya watu wenye asili ya Afrika limo katika majukumu ya baraza hilo, na linapaswa kulichunguza.
''Kwa bahati mbaya, kifo cha George Floyd siyo tukio pekee, kwa sababu watu wengi weusi wanakutwa na madhila yale yale kila siku katika sehemu nyingi za dunia. Wanakumbwa na ukatili wa polisi kwa sababu tu ya asili yao. Itakuwa haieleweki ikiwa baraza hili halitalishughulikia tatizo hilo,'' amesema Sougouri.
Sougouri alisema hiyo ndio sababu mataifa ya Afrika yanalitaka baraza hilo kuanzisha haraka mjadala kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu kwa misingi ya rangi ya ngozi, ubaguzi wa rangi wa kimfumo, na ukandamizaji wa polisi dhidi ya watu wenye asili ya Afrika wanaoandamana kupinga unyanyasaji dhidi yao.
Marekani so tena mwanachama
Marekani inayolengwa katika waraka huo sio mwanachama tena wa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa. Ilijiondoa miaka miwili iliyopita, ikidai baraza hilo lina uhasama dhidi ya Israel ambaye ni mwandani wa Marekani. Bado Washington waijatoa tamko lolote kuhusu hatua hiyo ya kuwekwa kizimbani.
Maudhui ya waraka wa nchi za kiafrika, ambayo yanaweza kurekebishwa baada ya mazungumzo ndani ya baraza, yanataka iundwe tume huru ya kimataifa itakayofanya uchunguzi wa masuala yanayohusu mifumo ya ubaguzi, uvunjaji haramu wa haki za msingi za binadamu, na unyanyasaji dhidi ya watu weusi nchini Marekani, na pia katika maeneo mengine ya dunia.
Tume hiyo itachunguza pia namna serikali na tawala za kimajimbo zinavyoshughulikia maandamano ya amani, na pia tuhuma za kutumia nguvu za ziada dhidi ya waandamanaji, watazamaji wa maandamani na waandishi wa habari.
Marekani na nchi nyingine zimetakiwa kutoa ushirikiano kamili na tume hiyo, inayopaswa kuchapisha ripoti yake baada ya mwaka mmoja.
Vyanzo: (rtre, ape)