Afrika yashauriwa kukuza kilimo cha kisasa
22 Januari 2018Naibu waziri mkuu na kiongozi wa shughuli za serikali katika bunge la Uganda, Jenerali Mstaafu Moses Ali amesema ili kuwepo na ustawi wa kilimo Afrika ni sharti wakulima waanze kutumia mbinu za kisasa na teknolojia katika shughuli zao za ukulima.
Jenerali Moses Ali ameeleza kwamba Afrika ina utajiri wa kutosha wa rasilimali za kilimo kwa hiyo inahitaji washirika wazuri tu watakaosaidia katika masuala ya kupenyeza teknolojia katika kilimo barani humo kutokana na ukweli kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa idadi kubwa ya nchi za Afrika.
Amezungumzia pia suala la ubora wa bidhaa kutoka Afrika akisema nchi nyingi za Afrika hazina teknolojia ya kutathmini ubora wa bidhaa za kilimo au hata kama ipo basi si ya kisasa.
"Teknolojia inaweza kusaidia, kwanza kuwapunguzia wakulima mzigo wa kutumia jembe, mtu anatumia jembe kwa kulimia chakula cha familia yake, na wengine hata kwa kuuzia nchi nzima. Hilo hata haliwezekani.
Ulimwenguni kwa sasa kilimo kinafanywa kwa mbinu za kisayansi, ambazo nafikiri iwapo hata sisi tutazifuata, tutakuwa kama wao, au hata kuwapita baadhi yao," alisema Jenerali Ali katika mahojiano na DW mjini Berlin.
Kinachotakiwa kwa sasa...
Katibu mkuu wa wizara ya kilimo nchini Uganda Pius Wasabi Kasajja alikuwa sehemu ya ujumbe wa Uganda uliohudhuria mkutano huo na amesema wakati umewadia kwa wakulima wa Afrika kuacha kufanya kilimo cha kukidhi mahitaji yao na familia zao tu bali wafanye kilimo cha biashara kitakachozinufaisha nchi zao pia.
Kassajja ameongeza hata hivyo, kwamba hilo litawezekana tu iwapo Afrika itashikwa mkono na wafadhili na wawekezaji kutoka nchi zilizoendelea. "Tunachohitaji kufanya kwanza ni kuwapanga wakulima wetu, kwa sababu kwa sasa hawana kitu wanachokifanya," alisema katibu mkuu huyo.
"Tunapaswa kuwaweka wakulima katika ushirika kuhakikisha kuwa wanazalisha chakula kwa ajili ya biashara, na kuwapa mwelekeo na vifaa vinavyostahili, tena vya kisasa na kwa kutumia teknolojia tunaweza kuzalisha chakula kwa wingi wa kutosha," alisema Kasajja.
Ujerumani kuipiga jeki Afrika
Wakati huo huo waziri wa kilimo wa Ujerumani Daktari Herman Onko Aeikens amesema kwamba Ujerumani iko tayari kuisaidia Afrika kwa kuwa mustakabali wa bara hilo unategemea maendeleo katika kilimo.
Daktari Herman ameonya lakini kwamba Afrika ni sharti ichukue jukumu kama bara na kwamba Ujerumani italishika mkono katika masuala kadhaa kama ufadhili na teknolojia, akisema ustawi na ufanisi wa kilimo unawategemea Waafrika wenyewe.
Waziri huyo pia ameelezea matumaini ya Afrika kupiga hatua katika kukabiliana na ufisadi ambao umeathiri sekta ya kilimo pia. Amezungumzia hatua ya viongozi wa nchi mbalimbali Afrika kupitia Umoja wa Afrika, kujitolea katika kukabiliana na ufisadi katika nchi zao akisema hiyo ni hatua itakayosaidia siyo kilimo tu bali hata uchumi wa Afrika.
Mwandishi: Jacob Safari
Mhariri:Iddi Ssessanga