Afrika: Visa vya COVID-19 vyapindukia milioni moja
7 Agosti 2020Kulingana na takwimu za shirika la habari la Reuters, hadi kufikia Ijumaa bara la Afrika limerekodi visa 1,003,056 vya maambukizi ya virusi vya Corona, na vifo 21,983 kutokana na ugonjwa wa COVID-19. Watu 676,395 wamepona ugonjwa wa COVID-19, shirika hilo limeongeza.
Afrika Kusini ambayo ni nchi ya tano katika mataifa yalioaathirika zaidi na virusi vya Corona kote duniani, imerekodi zaidi ya nusu ya maambukizi yote barani Afrika.
Kwa mujibu wa wizara ya afya ya Afrika Kusini, tangu kuripoti kisa chake cha kwanza mnamo Machi 5 nchi hiyo imerekodi visa 538,184 vya COVID-19 hadi kufikia sasa.
Hata hivyo wataalamu wanasema huenda idadi ya maambukizi barani humo ni kubwa zaidi ikiligansiha na idadi inayoripotiwa.
Wanasema hii ni kutokana na mataifa mengi barani Afrika isipokuwa Afrika Kusini kukosa vifaa vya kutosha kufanya vipimo vya virusi vya Corona na kueleza kuwa huenda bado kuna visa vingi ambavyo havijagunduliwa barani humo.
Mataifa mengi barani Afrika awali yaliweka mikakati kadha ya kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya COVID-19, ikiwemo kuwataka raia wake kusalia majumbani, kufunga mipaka yao pamoja na kufanya upimaji wa virusi hivyo.
Hata hivyo, athari kwa uchumi na hofu ya kutokea kwa baa la njaa vimesababisha nchi hizo kuanza kulegeza baadhi ya vikwazo hivyo kama zuio la kutotoka ndani. Wataalamu wanasema janga la COVID-19 limeanza kusambaa kwa haraka barani humo.
Huduma za afya Afrika Kusini kuzidiwa
Afrika Kusini, nchi yenye huduma bora zaidi za afya barani Afrika, awali ilionekana kufanikiwa katika kukabiliana na virusi vya Corona.
Shirika la habari la Reuters linaripoti kuwa kwa sasa mfumo wa afya wa nchi hiyo unaelekeaa kuzidiwa hasa kutokana na idadi kubwa ya visa vya COVID-19, uhaba wa vitanda vya wagonjwa pamoja na wahudumu wa afya kukosa vifaa vya kutosha kujikinga dhidi ya virusi hivyo hatari.
Nako nchini India takribani wahudumu wa afya 900,000 mnamo Ijumaa wameanza kushiriki mgomo wa siku mbili, wakilalamikia kile wanachosema ni kukosa vifaa vya kujikinga dhidi ya COVID 19, ili hali wanafanya kazi katika mazingira hatari ya kuambukizwa na virusi vya Corona. Kwa mujibu wa mwandaalizi wa mgomo huo AR Sindhu wahudumu hao pia wanataka kuongezewa malipo.
Hayo yakijiri, idadi ya maambukizi nchini humo imepita milioni 2 huku watu 41,000 wakifariki dunia kutokana na ugonjwa wa COVID-19.
Kwa mujibu wa wizara ya afya nchini humo, katika muda wa saa 24 ziliopita, nchi hiyo imeripoti visa 62,538 vya maambukizi ya virusi vya Corona na hivyo basi kujumuisha idadi jumla ya maambukizi nchini humo kuwa 2,027,074.
Kulingana na wizara hiyo pia, watu 886 wamekufa kutokana na COVID-19 na kufanya idadi ya vifo kupindukia 41,585.