Afrika na uchaguzi wa Marekani
1 Novemba 2012Lakini badala ya kulishika bara hilo kwa mkono wenye matumaini, Afrika ilipata sera kali na za kikaidi za "usalama kwanza".
Bara la Afrika lilijionesha wakati wa kuchaguliwa kwa Barack Obama kuwa rais wa Marekani Novemba 2008 kuwa lilifurahishwa mno. Waziri wa mambo ya kigeni wa Nigeria alitokwa na machozi, Nelson Mandela aliusifu uchaguzi huo na kusema kuwa ni thibitisho kuwa watu wanapaswa "kujaribu kuota ndoto," na Kenya ilitangaza kuwa ni siku ya mapumziko ya taifa.
Furaha hiyo haraka ilijibiwa kwa ziara ya Obama nchini Ghana miezi mitano tu baada ya kuapishwa.
Damu ya Mwafrika
"Nina damu ya Afrika," amesema Obama kwa hisia kali , alipolihutubia bunge la Ghana na watu waliokuwa wakitazama televisheni katika bara la Afrika. Afrika , rais huyo mpya alisema, sasa ni sehemu muhimu ya ulimwengu wetu uliounganika.
Lakini wakati mdororo mkubwa wa uchumi nchini Marekani ulipoongozeka , vita nchini Iraq na Afghanistan zikiendelea na likazuka vuguvugu la mapinduzi katika mataifa ya Kiarabu, mataifa ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara yakajikuta katika hali ambayo si ya kawaida, yakifichwa nyuma ya mambo yote hayo.
"Kulikuwa na matumaini kuwa atakuwa rais wa Marekani kwa ajili ya Afrika," amesema mwanadiplomasia wa siku nyingi nchini Afrika kusini Thomas Wheeler, hivi sasa akifanyakazi katika taasisi ya Afrika kusini ya masuala ya kimataifa. "Yalikuwa ni matarajio yasiyowezekana."
"Ukweli kwamba baba yake alitoka Afrika haukuwa na maana kuwa atatumia muda mwingi akihusika na Afrika."
Kimsingi, ziara ya Obama nchini Ghana ilikuwa ndio ziara yake pekee katika eneo hilo. Pamoja na hayo kimsingi , ilichukua hadi Juni mwaka huu kwa Ikulu ya Marekani ya White House kuja na waraka wenye kurasa tisa , juu ya "mkakati wa Marekani kuhusiana na mataifa ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara".
Hata hivyo bara hilo halikutupwa kando
Ndege ya rais Air Force One haijaonekana tena katika bara la Afrika, lakini ndege za jeshi la anga la Marekani , pamoja na matawi mengine ya huduma za usalama nchini Marekani zimeonekana katika bara hilo.
Kimya kimya , sera za Marekani kuelekea bara la Afrika zilianza kuonekana kuchukua mkondo mkali zaidi na zaidi , kama vile zilivyo sera kuelekea duniani kote.
"Obama kwa akili yangu analishughulikia zaidi bara la Afrika, lakini kiini cha jinsi gani Marekani inashughulika katika bara la Afrika kimebadilika. Kumekuwa na mwelekeo zaidi wa kiusalama," amesema Jason Warner, mtaalamu wa chuo kikuu cha Harvard ,kuhusu usalama katika bara la Afrika.
Kwa mujibu wa Warner, Obama amesaidia katika kuweka katika hali ya kawaida ,sera kuelekea Afrika. "Hakuna eneo jingine duniani ambalo Marekani inajihusisha kwa misingi ya ubinadamu tu."
Tangu pale Obama alipochukua madaraka imeripotiwa kuwa utawala wake umepanua mtandao wa vituo vya jeshi la anga katika bara hilo, wakitunisha misuli yao dhidi ya makundi yenye mafungamano na kundi la kigaidi la al-Qaeda pamoja na makundi mengine.
Vituo vya siri nchini Burkina Faso, Mauritania na Uganda vinasemekana kutumiwa kwa njia kadha kufanya upelelezi dhidi ya al-Qaeda katika eneo la maghreb la mataifa ya Kiislamu na kuwafuatilia baadhi ya watu wanaohusika na kundi la Lord's Resistance Army, linaloongozwa na Joseph Kony.
Mashambulizi ambayo hayajathibitishwa na ndege zisizokuwa na rubani yameripotiwa mara kwa mara nchini Somalia. Kwa mujibu wa ofisi yenye makao yake makuu mjini London ya uandishi wa habari za kiuchunguzi , kati ya watu 58 na 170 wameuwawa katika mashambulio kati ya 10 hadi 23 nchini Somalia, licha ya kuwa baadhi yamefanyika wakati wa utawala wa rais wa zamani George Bush.
Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe
Mhariri: Mohammed Khelef