1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS yawawekea vikwazo watawala wa kijeshi Guinea

17 Septemba 2021

Wakuu wa mataifa ya Afrika Magharibi wametangaza vikwazo dhidi ya viongozi wa mapinduzi nchini Guinea, na kutaka uchaguzi uitishwe katika miezi sita ili kurejesha haraka utawala wa kiraia baada ya mapinduzi ya mwezi huu.

https://p.dw.com/p/40QrA
Ghana l Sitzung der Wirtschaftsgemeinschaft Westafrikanischer Staaten (ECOWAS) zur politischen Lage in Guinea
Wakuu wa mataifa ya kanda ya Afrika Magharibi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano wa kilele mjini Accra, Ghana, Septemba 16, 2021, walikozungumza juu ya hali nchini Guinea.Picha: Nipah Dennis/AFP

Wakuu hao wa mataifa wameamua kuzuwia mali za kifedha na kuwawekea marufuku ya kusafiri wanachama wa utawala wa kijeshi na ndugu zao, huku wakisisitiza juu ya kuachiliwa kwa rais Alpha Conde.

Rais wa jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS, Jean Claude Brou alisema viongozi wakuu wa mataifa ya Afrika Magharibi wamesisitiza pia kwamba hakupaswi kuwepo na haja ya kipindi kirefu cha mpito kwa taifa hilo kurejea kwenye mkondo wa kidemokrasia.

"Kipindi cha mpito laazima kiwe kifupi, na wamesisitiza hata kwamba hakipaswi kudumu zaidi ya miezi sita, hivyo katika miezi sita, uchaguzi unapaswa kufanyika.

Soma pia: Watawala wapya Guinea watafuta kujiimarisha madarakani

Wanasisitiza hilo kwa sababu uchuguzi utaruhusu kurejeshwa kwa utaratibu wa kikatiba katika jamhuri ya Guinea," alisema Brou katika taarifa.

Guinea Junta
Kiongozi wa kijeshi wa Guinea Luteni-Kanali Mamady Doumbouya, katikati, akiwa amezungukwa na walinzi baada ya mkutano na wajumbe wa ECOWAS mjini Conakry, Guinea, Ijumaa Septemba 10,2021.Picha: Sunday Alamba/AP/picture alliance

Shinikizo la kuachiwa Alpha Conde

Vikwazo hivyo vinavyolenga watu makhsusi vinakuja baada ya viongozi wa mapinduzi kutaja masharti kadhaa ya kumuachia Conde, kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Ghana.

Tayari ECOWAS ilikuwa imeonya kwamba ingewaadhibu watawala wa kijeshi endapo hawangemuachia Conde, ambaye anazuwiliwa katika eneo lisilojulikana tangu alipokamatwa wakati wa mapinduzi ya Septemba 5 mjini Conakry.

Soma pia: Umoja wa Afrika waisimamisha uanachama Guinea kwa muda

ECOWAS imetoa wito pia kwa Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya kuunga mkono vikwazo dhidi ya utawala wa kijeshi, unaojulikana kama Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano na Maendeleo au kwa kifupisho chake cha Kifaransa CNRD.

ECOWAS ilikuwa imetuma ujumbe nchini Guinea wiki iliyopita kukutana na kiongozi wa mapinduzi Luteni Kanali Mamady Doumbouya, na ilikuwa inasubiri kuchukuwa uamuzi juu ya namna ya kuushinikiza utawala wa kijeshi kurudi kurudi kwenye utawala wa kikatiba.

Guinea ECOWAS-Delegation in Conakry
Wajumbe wa ECOWAS wakiwa katika mkutano na utawala wa kijeshi wa Guinea mjini Conakry, Septemba 10, 2021.Picha: Präsidentschaft Guineas

Mashauriano ya kitaifa Guinea

Siku ya Jumanne, utawala wa kijeshi ulianzisha mazungumzo ya siku nne pamoja na makundi mbalimbali kujadili njia ya kurudi kwenye utawala wa kiraia.

Luteni-Kanali Doumbouya na maafisa wake wamekutana mpaka sasa na viongozi wa kisiasa, mamlaka za kidini na wanaharakati wa haki za binadamu, na walitarajiwa kuzungumza na wanadiplomasia wa kigeni, vyama vya wafanyakazi na watendaji wa sekta ya madini siku ya Ijumaa.

Soma pia: Jeshi la Guinea laanza kujadili mustakabali wa taifa hilo

Wakuu wa mataifa pia wameongeza mbinyo dhidi ya serikali ya mpito ya Mali, wakiitaka kuheshimu makubaliano ya kuandaa uchaguzi wa Februari 2022, na kuwasilisha mpango wa uchaguzi kufikia mwezi ujao, kwa mujibu taarifa ya baada ya mkutano wa kilele wa jana.

Chanzo: Mashirika