Kuta ya ANC yamalizika
18 Desemba 2017Wagombea wa kinyanga'nyiro hicho ni Makamu wa Rais Cyril Ramaphosa na mke wa zamani wa Rais Jacob Zuma na ambaye pia ni waziri wa zamani, Nkosazana Dlamini-Zuma.
Upigaji kura ulianza usiku wa manane Jumapili na kuendelea hadi asubuhi Jumatatu kufuatia ucheleweshaji wa mara kwa mara unaotokana na mzozo juu ya wajumbe wanaostahili kupiga kura, huku mamia ya watu waliohudhuria wakizuiwa kushuhudia kura hiyo.
Hadi Jumatatu asubuhi, wajumbe wengi miongoni mwa 4,776 walikuwa tayari wameshapiga kura.
Matokeo yanatarajiwa kutolewa baadae lakini bado haikuwekwa wazi uhesabuji kura utachukuwa muda gani.
Msemaji mkuu wa chama cha ANC, Khusela Sangoni, amewaambia waandishi wa habari kwamba mchakato huo unaendelea vizuri.
Wananchi wa Afrika Kusini wana matumaini kwamba yeyote kati ya wagombea hao wawili atakayeshinda ataleta uongozi mpya ndani ya chama cha ANC, baada ya kashfa za rushwa zilizoleta uharibifu chini ya uongozi wa Rais Jacob Zuma.
Kiongozi mpya wa chama hicho ndiye atakayegombea uchaguzi ujao wa rais 2019, na licha ya kuwepo madarakani kwa miaka 23, ANC bado kina umaarufu nchini Afrika Kusini.
Hata hivyo, asilimia 54 iliyoshinda katika uchaguzi wa mitaa mwaka jana ilikuwa ni matokeo yake mabaya zaidi tangu 1994.
Na umaarufu huo umepungua ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Chama cha ANC kimeongoza tokea mwaka 1994 pale Nelson Mandela aliposhinda kura ya kwanza nchini humo iliyojumuisha watu wa rangi tofauti, wakiwamo watu weusi.
Zuma ambaye utawala wake umechafuliwa jina na kashfa kadhaa, ataachia madaraka kama kiongozi wa chama cha ANC lakini ataendelea kuwa kiongozi wa nchi hadi pale utakapofanywa uchaguzi mkuu wa rais mwaka 2019.
Zuma amekabiliwa na madai ya rushwa tangu alishika madaraka kama kiongozi wa nchi mwaka 2009, lakini kiongozi huyo amekataa makosa yoyote.
Kwa upande wa upinzani, vyaama vya Democratic Alliance na Economic Freedom Fighters winatarajiwa kupambana na chama cha ANC na huenda vikakubaliana kuunda serikali ya mseto iwapo vitashinda katika uchaguzi ujao.
Kuongezeka kwa ukosefu wa ajira na ufisadi ndani ya serikali kumesababisha hasira dhidi ya chama cha ANC miongoni mwa wananchi maskini wa Afrika Kusini, ambao wanaishi katika makaazi mabaya, elimu duni, na ukosefu wa usawa miongoni mwa watu wa rangi tafauti.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/afp/dpa/rtre
Mhariri: Mohammed Khelef